Tafauti ya maendeleo ya fasihi andishi ya Zanzibar kabla ya
uruhu na baada ya uhuru katika vipengele vya Hadithi fupi, Riwaya, Ushairi na
Tamthilia ni kama ifuatavyo. Tutajadili kwanza Riwaya, pili Ushairi tatu
hadithi fupi na mwisho ni tamthilia.
Riwaya.
Kwa mujibu wa Wamitila (2003)
anasema riwaya ni kazi ya kinathari au kibunilizi ambao huwa na urefu wa
kutosha, msuko uliojengeka vizuri, wahusika wengi walioendelezwa kwa kina,
yenye kuchua muda mwingi katika maandalizi na kuhusisha mandhari maalumu.
Mkwera (1978) anasema
kuwa riwaya ni hadithi iliyo ndefu kuweza kutosha kufanya kitabu kimoja au
zaidi.
Muhando na Balisidya. (1976) wanaeleza riwaya ni kazi ya
kubuni, ni hadthi ambayo hutungwa kufuatana na uwezo wa fanani kuibusha mambo
kutokana na mazoea au mazingira yake. Wanaendelea kusema kuwa riwaya yaweza
kuanzia maneno 35000 hivi na kuendelea.
Ukubwa wa riwaya, unaweza kuwa wa kurasa zozote zile kwani
si idadi ya maneno au kurasa tu ambavyo vitatufanya tuiite hadithi fulani kuwa
ni riwaya na nyingine kuwa hadithi fupi, zipo riwaya kana Nyota ya rehema
(1981) kuli (1979)
Tukianza kuzungumzia historia ya riwaya ya Kiswahili ni
muhimu kuihusisha sana na fasihi simulizi. Uhusiano huu sio wa kimuundo, ingawa
muundo wa masimulizi ulichangia kwa kiasi fulani katika riwarya nyingi za
mwanzo, lakini zaidi ni uhusiano uliotokana na uandikaji wa hadithi za
Kiswahili. Edward Steere alipokusanya na kuhariri hadithi alizozipata kutoka
kwa wakazi hadithi alizozipata tutoka kwa wakazi wa Zanzibar unaweza kuwa ndio
wakati wa kwanza kuangalia histori ya riwaya yetu ya Kiswahili (Mlacha na
Madumulla, 1991:11).
Kwa mujibu wa Mulokozi anasema kuwa chimbuko la riwaya lipo
katika mambo makuu mawili
Moja ni fani za kijadi za fasihi na
pili ni mazingira ya kijamii
Fani za kijadi kama vile:-
Ngano-hadithi za kubuni zinazohusu
wanyama, watunzi wengi wameathiriwa na ngano kw wasababu wanachota visa, mbinu
za kifani , dhamira katika ngano (zinaonekana kwamba ni za kingano zaidi)
Visasili-masimulizi ya kubuni ambayo
yanaeleza juu ya maisha, asili, ya vitu na hatima yake. Kwa kawaida visasili
huaminiwa kuwa ni hadithi za kweli
Visakale
ni hadithi za kale kuhusu mashujaa wa taifa, kabila au dini. Mara nyingi visa
kale huchanganywa na historia na masimulizi ya kubuni na hadithi hizi
hupatikana katika kila kabila au kila lugha. Baadhi ya visa kale vya Kiswahili
ni masimulizi kuhusu miji ya pwani na Zanzibar. Mfano mzuri ni hadithi ya
Abdallah Bin Hemed bin Ali Ajjemy (1972)
Hekaya-ni hadithi za kusisimua kuhusu
masaibu na matukio ya ajabu yasiyo ya kawaida, mara nyingi masaibu
yanasababishwa na mapenzi, huwa ni ndefu kuliko hadithi nyingine lakini si
ndefu kuliko riwaya.
Tendi-ni hadithi ya kishairi kuhusu
mashujaa wa kihistoria na wakubuni wa jamii au taifa
Masimulizi
ya wasafiri. Hizi ni habari zinazosimulia masaibu ya wasafiri katika nchi mbali
mbali. Hizi nazo zilisaidia kupatikana kwa riwaya. Mfano Alfa-lela-ulela.
Katika karne ya 16 fani nyingi ziliendelea. Na
mojawapo ya sababu ya kuendelea kwa riwaya ilikuwa ni:
Ukuaji mkubwa wa shughuli za kiuchumi
huko Ulaya baada mapinduzi ya kiviwanda
Mageuzi ya kijamii na kisiasa
yaliyofungamana na mabadiliko ya kiuchumi
Ugunduzi wa teknolojia ya upigaji chapa
Maendeleo ya riwaya kabla ya uhuru Zanzibar.
Tukianza kuzungumzia historia ya riwaya ya Kiswahili za
Zanzibar ni muhimu kuhihusisha sana na fasihi simulizi. Uhusiano huu sio wa
kimuundo, ingawa muundo wa masimulizi ulichangia kwa kiasi fulani katika
riwarya nyingi za mwanzo, lakini zaidi ni uhusiano uliotokana na uandikaji wa
hadithi za Kiswahili. Edward Steere alipokusanya na kuhariri hadithi
alizozipata kutoka kwa wakazi wa Zanzibar unaweza kuwa ndio wakati wa kwanza
kuangalia histori ya riwaya yetu ya Kiswahili (Mlacha na Madumulla, 1991:11).
Kwa hivyo tukiichambua nukuu hiyo tunaweza kusema kuwa historia ya riwaya za
Zanzibar na maendeleo yake ilianzia karne ya 18 mara tu Bw. Edward Steere
alipokusanya na kuhariri hadithi alizozipata kutoka kwa wakazi wa Zanzibar.
Kabla ya ukoloni sehemu kubwa ya fasihi andishi ya
kimasimulizi ilikuwa ni tendi. Baadhi ya tendi hizo ni kama vile kisa cha
Anzaruni au Siri lAsirari Binti Lemba:1663) Kadhi Kassim bin Jaafar Hemed
Abdalla karne ya kumi na 9 zilitumia mbinu za kiriwaya kwa mfano ubunifu wa
vituko, msuko na matukio ambazo ziliandaa mazingira ya kisanaa yaliyochangia
kuzuka kwa riwaya.
Jambo jengine lililosaidia kuchipuza kwa riwaya Zanzibar ni
tafsiri. Tafsiri za mwanzo katika lugha ya Kiswahili zilikuwa za kidini kwa
mfano tafsiri ya kwanza iliyofahamika ni Sayyid Aidarus Bin Athuman karne 17.
Kaswida ya Hamziyah 1652. Pia vilitafsiriwa vitabu vya hadithi kutoka lugha ya
kiarabu kwa Kiswahili Mfano Hekaya Abunuasi na Alif-Lela-Ulela.
Kuundwa kwa kamati ya lugha ya Afrika mashariki mnamo mwaka
1929, kazi ya Kamati hii ilikuwa na nafasi kubwa sana katika kuendeleza lugha
ya Kiswahili na fasihi ya Kiswahili. Na bila ya shaka iliendeleza riwaya za
Zanzibar. Kamati pia iliandaa mashindano ya uandishi wa kazi za fasihi. Hali
hii ilisababisha kutokea kwa waandishi wapya wa riwaya. Mfano wa mwandishi
mashuhuri wa riwaya Muhammed Said Abdulla (BWANA MSA) na vitabu vyake kama vile
Mzimu wa Watu wa Kale.(1958), Kisima cha Giningi (1958).
Mwandishi mwengine wa riwaya za Zanzibar zilizoandikwa kabla ya uhuru ni
mwandishi Muhammed, M. S na kitabu chake cha Kurwa na Doto (1960) katika
kipindi hiki waandishi hasa wamezingatia namna jamii ilivyokuwa kabla ya uhuru
Mfano: Mzimu wa watu wa kale kilikuwa na maudhui ya athari ya dhulma na
upepelezi, Kurwa na Doto thamani ya utamaduni katika jamii mila na
utamaduni. Na Kisima cha Giningi ni uongozi mbaya na ushirikina.
Baada ya uhuru riwaya za kiswahi zikiwemo za Zanzibar
zilipevuka na kutanuka zaidi na hii ilikuwa kwenye miaka ya 1970-1975 kadhalika
zilijitokeza riwaya za mikondo mbali mbali mambo makuu yaliyoipambanua riwaya
ya Kiswahili ni
Moja kutokea kwa watunzi wapya vijana ambao wameipa uhai
mpya riwaya Mfano Said Ahmed Muhamed, Shafi Adam Shafi Muhamed S. Abdulla.
Pili kuongezeka kwa riwaya pendwa ambako kuliambana na kutokeza
kwa wachapishaji ambao walichapisha riwaya zao wenyewe.
Tatu kujitokeza kwa riwaya inayoihakiki jamii kwa undani
ambazo wengine waliziita riwaya za uhalisia. Baadhi ya watunzi mashuhuri ni
Shafi Adam Shafi na Kasri ya Mwinyi Fuadi(1978) na Kuli (1979),
S, A Muhamed na Tata za Asumini (1990).
Nne kuzuka kwa riwaya za kihistoria mfano wa riwaya hizo ni Vutan’kuvute
ya mwandishi Shafi Adam Shafi (1999).
tano kuanzishwa kwa taaluma ya uhakiki wa fasihi ya
Kiswahili. Taaluma hiyo ilianza kufundishwa baada ya kuanzishwa kwa idara ya
Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam mnamo mwaka 1968-1970. Taaluma
hii ilienezwa hadi mashuleni. Mulokozi, M.M(1996).
Ushairi.
Ushairi kwa mujibu wa Massamba
D.P.B (2003) akimnukuu Shaaban Robert anasema ushairi ni Sanaa ya vina
inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi Zaidi ya kuwa na Sanaa ya vina
ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari.
Mnyampala (1970)
anasema kuwa ushairi ni msingi wa maneno ya hekma tangu kale ndicho kitu
kilichobora sana maongozo ya dunia kwa kutumia maneno ya mkato na lugha nzito
yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa mizani na vina maalum.
Amri Abeid (1954:1) anasema kuwa ushairi au utenzi ni wimbo
hivyo kama shairi haliimbiki halina maana.
Chimbuko la ushairi. Katika kipengele hiki kuna nadharia
nyingi zinazoeleza juu ya chimbuko la ushairi wa Kiswahili.
Kuna nadharia inayosema kwamba ushairi wa Kiswahili chimbuko
lake ni ujio wa waarabu, na nadharia nyengine ni ile ya ushairi kuwa ni zao la
jamii ya waswahili wenyewe.
Nadharia ya pili ni ile ya ushairi chimbuko lake ni zao la
waswahili wenyewe. Katika nadharia hii tunaweza kungundua kuwa ushairi hapo
kale ulikuwepo hata kabla ya ujio wa wakoloni na ndio kipindi cha ushairi kabla
ya uhuru. Nadharia hii imejadiliwa na wataalamu mbali mbali wakiwemo Shaban
Robert, Jumanne Mayoka (1993) na F.E.M.K Senkoro, Mulokozi na Sengo. Tukianzia
na Jumanne Mayoka (1993), yeye anasema kuwa ushairi umetokana na jamii ya wanaadamu
wenyewe na umesheheneza ukwasi mkubwa wa lugha ambayo imekuwa ikitumika katika
hatua zote za kisiasa, kiuchumi, na kiutamaduni katika historia ambayo
mwanaadamu amepita. Kwa mfano kuwa msamiati uliotumika tangu enzi za kuishi
mapangoni, enzi za uwindaji, ujima, utumwa, vita vya makabila au uvamizi wa
wageni, ukoloni na harakati za kupambana na ukoloni hadi uhuru na maendeleo
yake.
Senkoro (1988) anasema kuwa ushairi uliibuka pale lugha
ilipoanza katika kipindi cha uhayawani (Kipindi ambacho mwanaadamu alipoanza
kupambana na mazingira yake) kwenda katika kipindi cha urazini (maana)ili
kumuezesha mwanaadamu na mazingira yake. Kwa Mfano zana za kazi zilizotumika
ziliwafanya waimbe kwa kufuata mdundo wa zana hizo.
Tukiziangalia nadharia hizi mbali zinatuelekeza kuwa
Zanzibar nayo ni miongoni mwa sehemu za pwani ya Afrika Mashariki ambako ndiko
kunakopatika ushairi wa Kiswahili. Hivyo kwa namna yeyote ile imepitia historia
hiyo na mabadiliko yake. Katika kulibainisha hili kuhusu hoja ya ushairi ni zao
la waswahili wenyewe hata wazanzibari kuna nyimbo zilitumika katika
kuwabembelezea watoto mfano wa nyimbo hiyo inasema:-
Owa mtoto owa, owa mtoto owa
Silia mwanangu silie, ukaniliza na mie
Machozi yako yaweke, nikifa unililie
Jipigepige makonde, watu wakushikilie
Kinoleo cha maboga, kutia nazi kunoga
Mkono wataka kula, maungo yaona woga
Kile kidau kijacho, hakikosi mna changu
Mna mkufu mpambe, kadiri ya shingo yangu
Aupata siuvai, wala simpi mwenzangu
Nampelekea mama, msiri wa mambo yangu
Owa owa mtoto owa, owa owa mwanangu owa
Kilelema kilelema, kitawi cha mlelema
Ukakichuma cha juu, cha chini kitakulema
Mti mshindao nyani, ujuwe una kilema…..
Wimbo huu hadi hii leo wanajamii wa Zanzibar wanaendelea
kuutumia kwa shughuli ile ile ya malezi kwa watoto ambayo wazee wao waliitumia
kuwalelea watoto wao.
Tukiangalia katika nadharia ya kwanza kuwa ushairi ulitokana
na ujio wa waarabu. Hoja hii inatufungua macho kwamba ushairi inawezekana
kwamba ulikuja enedelezwa baada ya ujio wa wageni. Kwa muktadha huu basi
tunasema kuwa Zanzibar ni miongoni mwa maeneo yaliyowahi tawaliwa na waarabu
kutoka Oman. Hoja hii imeungwa mkono na wataalamu mbali mbali kama vile Lyndon
Harries (1962) katika kitabu chake kiitwacho Swahili Poetry anatoa
ushahidi kuwa ushairi wa Kiswahili ulitokana na uislamu. Yeye anasema kuwa
ushairi ulianzia kwenye upwa wa kaskazini mwa Kenya hususan Lamu. Utungo wa
kwanza wa ushairi andishi wa Kiswahili ni Tambuka , Mwengo bin Athman
(1728),waandishi wengine waliotunga tenzi miaka ya baadae baada ya hiyo ni
mwandishi Chum Haji na utenzi wake uitwao Utenzi wa vita vya Uhudi (1962).
Ushairi ulipita katika hatua mbali mbali katika maendeleo
yake katika kipindi hiki baada ya ujio wa wageni inasemakana ilikuwa ni kipindi
cha Utasa kama asemavyo Kezilahabi(1983) yeye alisema kuwa kipendi hiki
kilikuwa kati ya (1885-1945) katika kipindi hiki ushairi umekubwa mabadiliko ya
kiutawala na kielimu na ilikuwa ni kubadilika kwa hati za Kiarabu kuwa za
Kirumi. Kwa hovyo washairi wengi nao walikubwa na mkumbo huo.
Ushairi ulishamiri baada ya uhuru kwa kuzuka mashairi mbali
mbali yaliyojikita katika siasa za kujitawala baada ya kupatikana uhuru.
Waandishi wa Zanzibar nao hawakuachwa nyuma bali waliandika vitabu mbali mbali
vya mashairi vikiwa na dhamira kadhaa za kujitawala na za kidini pia. Mifano ya
kazi za kifasihi za kishairi baada ya uhuru Zanzibar ni Utenzi wa Rasil-ghuli
uliotungwa na Faqih Mgeni (1975), Fungate ya uhuru na Muhammed S. Kh (1975), Pambazuko (1982), Kimbunga
na Haji G. Haji (1995) na Malenga wapya (1997) kilichotungwa na
Takiluki.
Hadithi fupi.
Hadithi fupi. Msingi wa hadithi fupi ulianzishwa kwa kiasi
kikubwa na mtunzi na mhakiki maarufu wa kimarekani akijuilikana kama mwasisi wa
utanzu huu. Edgar Allan Poe pamoja na mhakiki maarufu kwa jina la Brander
Mathews ambae ndia inayoaminika kuwa ndie aliyetumia neno la Kingereza la
“Short Story” Hadithi fupi kwa mara ya kwanza.
K. W. Wamitila (2000) akimnukuu Mbatiah na yeye akiwanukuu akina Edger Poe kupitia
kitabu cha Tales kwa kusema:-
Hadithi fupi
si sura katika riwaya, tukio wala kituko ambacho kimechopolewa katika hadithi
fupi au kisa kirefu bali humvutia na kumteka msomaji na kumfanya aamini kuwa
ingeweza kuharibika ikiwa itakuzwa na kuwa ndefu au kama itafanywa sehemu ya
kazi kubwa.
Utanzu huu umekuwa sana, hasa kiuchapishaji katika fasihi za
lugha za ulaya ukilinganishwa na Kiswahili. Hata hivyo historia ya ukuwaji
wa utanzu huu ulimwenguni inalingana na kufafanana. Wandishi wengi wa hadithi
fupi walianza kuandika hadithi zao na kuzichapisha magazetini. Na hadithi
yengine zilishindanishwa katika idhaa ya B.B.C na hatimae kuchapishwa katika
mifululizo ya vipindi mbali mbali katika vyombo vya habari. Zanzibar ikiwa ni
sehemu ya wanajamii wa Kiswahili nayo haikuwa nyuma katika miaka ya sabiini Muhamed
S. A aliyeandika kitabu chake kiitwacho Kicheko cha Ushindi (1978).
Katika miaka ya themanini S. A Muhamed
na kitabu chake cha Si Wazimu si Shetani, Takiluki na kitabu chao cha
Hapa na Pale.
Katika kuendelea na utanzu huu wa hadithi fupi miaka ya hivi
karibuni waandishi wa Zanzibar waliendelea kuandika hadithi fupi wakiwemo Mw
Ali Mwalim Rashid na vitabu vyake kama vile Sungura na Mbweha, Safari
ya Hamadi vyote mwaka (2004), Haji Gora Haji na kitabu cha Nahodha Chui (2004).
Hii ndio historia fupi ya hadithi fupi Zanzibar.
Tamthiliya.
Nne kwa mujibu wa Mulokozi M (1996) tamthilia au drama ni
fani ya fasihi iliyokusudiwa kutendwa jukwaani kwa ajili ya hadhira fulani.
Wamitila (2004) tamthilia ni utanzu ambao hutegemea
mzungumzo na uigizaji ili kuwa silisha ujumbe wake..
Haji, A. I na wenzake (1981) wao wanasema kuwa tamthilia ni
utungo ulioandikwa au usioandikwa ambao unalieleza na kuliweka wazo linalotaka
kuwasilishwa katika hali ya kuweza kutendeka mbele ya hadhira.
Historia ya Tamthiliya kabla ya ukoloni Zanzibar haikuwepo ikiwa ni sehemu ya
Tanzania. Kulikwa na aina yengine tu za Sanaa za maonyesho ambazo ni kinyume na
tamthiliya ya hivi sasa iliyoingizwa na tamaduni ngeni. Kwa hivyo tunaweza
kusema kwamba tamthiliya ilianza nchini Tanzania mnamo miaka ya 1960. Katika
kipindi hiki bila ya shaka kulikuwa na tabaka mbili nazo ni tabaka tawaliwa na
lile tawala. Katika kuwatawala tabaka tawaliwa watawala walianzisha shule.
Shule ndio iliyokuwa silaha tosha kwa wakoloni kuwatawala wenyeji. Shule
zilitumika kuonesha tamthiliya zilizobeba itikadi za kibepari. Tamthiliya za
kingereza zilionyeshwa na zile za kihindi zilioneshwa pia. Tamthilia zote hizi
zililenga kuimarisha tamaduni ngeni. Waafrika hawakuwa na nafasi ya kusawiri
maisha yao. Mifano ya tamthilia zilizokuwepo wakti huo ni kama zile za
Shakespeare kama Hamlet, Macbeth, Romeo na Juliet na nyengine nyingi.
Vichekesho ni tamthilia za mwanzo zilizoanza baada ya
majilio ya wageni wananchi waliigiza vichekesho kwa kuamini kuwa ni kitendo
chenye kufurahisha na kuburudisha tu.
Katika miaka ya 1957 hadi 1960 vichekesho na tamthilia
fupifupi zilichezwa mashuleni hasa mwisho wa muhula au kwa mashindano baina ya
madarasa au siku za sherehe maalumu za shule hizo kama (siku ya wazazi).
Tamthiliya baada ya uhuru zilikuwa hasa ni kudumisha utamaduni
wa Mwafrika hap tamthilia nyingi zilitafsiriwa kwa Kiswahili kutoka Kingereza.
Tamthilia hizi zilikuwa manamo miaka ya
1969-1973. Baadhi ya tafsiri hizo ni Hakimu Mwadilifu
(1973) ya Evans Brother, Julius Kaizari (1969) J. K Nyerere na nyeinginezo. Hapa tamthiliya
ilichukuwa sura mpya kwani jamii nayo ilipaswa kujitawala wenyewe ili
kujiimarisha kiuchumi na kisiasa na kifikra pia. Taasisi mbali mbali
zilianzishwa ili kukuza na kuimarisha utamaduni wa Mtanzania akiwemo
Mzanzibari. BAKITA kwa upande wa Tanzania Bara na BAKIZA na TAKILUKI vyombo
vyote hivi vilianzishwa ili kukuza na kuendeleza waandishi wanaoandika katika
Kiswahili. Dhamira nyingi zilijitokeza ili kuakisi hali halisi ya wakati huo. Hapa
masanii Muhamed S. A zilipamba moto
zikiwemo Kivuli Kinaishi (1990), Amezidi(1995), Kitumbua
Kimeingia Mchanga (2000) na tamthilia ya Mazonge(2004) ya mwandishi
Ali Mw. Rashid.
Kwa muktadha huo tumeweza kuona maendeleo ya Fasihi Andishi
ya Zanzibar kabla ya majilio ya wageni vipengele(kama Hadithi fupi, Riwaya, Ushairi, Tamthilia) vyote
tulivyovijadili vilikuwa vya namna ya kienyeji vikiendana na amali za wenyeji
(Wazanzibar na Watanzinia kwa ujumla ) na baada ya uhuru ambapo vipengeli hivyo vilichota baadhiya
miundo na namna ya wasilishaji wake kuendana na hali ya jamii ilivyo kisiasa,
kijamii, kiuchumi na kitamaduni.
MAREJEO
Haji,
A. I na wenzake (1981) Misingi ya
Nadharia ya Fasihi: Berlin Arlov Sweden.
Madumulla, J.S(2009) Riwaya
ya Kiswahili, Historia ya Uchambuzi. Nairobi Sitima Printer and Stations
Ltd.
Mulokozi,M.M (1996) Utangulizi
wa Fasihi ya Kiswahili Dar-es-salaam, TUKI.
Nkwera F.V (1978) Sarufi
na Fasihi Sekondari na Vyuo . Dar-es-salaam Tanzania Publishing House.
Massamba. D. P.B (2003)Utunzi
wa Ushairi wa Kiswahili katika Makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa
Kiswahili (iii) Fasihi. Taasisi ya Uchambuzi wa Kiswahili Dar-es-salaam
Wamitila
K.W (2010) Kichoche cha Fasihi Simul izi na
Andishi, English Press. Nairobi.
Edwin
Semzaba(OSW 208) Tamthilia ya Kiswahili.
Chuo Kikuu Huria. Tanzania.