YALIYOMO
1.0 Utangulizi.
1.1
Miongoni
mwa tabia na mwenendo mwema unaosabisha mja kuipata shahada mwisho wa maisha
yake.
1.2
Matendo
mabaya na maovu yanayosababisha mja kukosa shahada wakati
wa kifo chake.
2.0 Hitimisho.
1.0
Utangulizi
Uislamu ni mfumo kamili wa maisha na ndio dini inayokubalika na
muumba wetu kama alivyosema katika Qur-ani kwamba dini anayoikubali M/Mungu ni
uislmau. Kupitia hadithi ya Mtume iliyotoka kwa Abdur-Rahman Abdullah bin Umar
bin Khattwab (r.a) anasema: Nimemsikia Mjumbe wa Allah (S.A.W) akisema “Uislamu
umejengwa juu ya mambo matano: kushudia ya kuwa hakuna mola apasaye kuabudiwa
kwa haki isipokuwa Allah na kuwa Muhammad ni Mjumbe wa Allah na kusimamisha
swala na kutoa Zaka na kuhiji Nyumba Tukufu, na Saumu ya Ramadhan.” (Bukhar
na Muslim). Tukiichunguza hadithi hii kwa makini inatuhakikishia kwamba “Kushudia
ya kuwa hakuna mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila ni Allah na kuwa Muhammad ni
Mjumbe wa Allah. Ndio nguzo ya kwanza inayousimamisha uislamu na mja hana budi
ili afanikiwe hapa duniani na akhera ni budi aishi kulingana na maamrisho
aliyoyaamrisha Allah na Mtume wake, na ayaepuke yale yote yaliyokatazwa na
Allah na Mjumbe wake.
Kwa mkabala wa kiislamu hakika hakuna tafauti ya dunia na dini ila
kuna mambo ya kiislamu na yasiyokuwa ya kiislamu. Bila ya shaka jambo ambalo
litaundwa kwa misingi ya kiislamu litakuwa la kiislamu kwa hivyo tamthilia ya
“Shahada” imejaribu kwa kiasi kikubwa kuonesha matendo mbali mbali ambayo mtu
akiyafanya huwa ni sababu mwisho wa maisha yake kuipata shahada na kuwa mja
mwema. Kinyume chake imejaribu kuonesha matendo maovu ambayo yatamfanya mtu
kujuta mwisho wa maisha yake na kuikosa shahada. Matendo hayo yameoneshwa kupitia
wahusika walioicheza tamthilia hiyo kama vile Salami (Mume wa Mama Afrah na
mwajiriwa wa Bw. Zuberi), Samira (Mke wa Zuberi), Zuberi (Mwajiri wa Salami),
Kifimbo (Rafiki wa Zuberi na Salami) na wengineo ambao wamebeba dhima mbali za
tamthilia hii.
Katika tamthilia ya
“Shahada” tunajifunza kwamba tabia njema ndio ufunguo wa kuipata shahada katika
maisha ya muislamu. Kama Mtume alivyowahimiza waumini kujipamba na tabia njema.
Kutoka kwa Abdalla bin Amr
(r.a) anaeleza kuwa Mtume wa Allah amesema “Aliyekipenzi changu kuliko wote
katika nyinyi (waislamu) ni yule aliyewazidi kwa tabia njema” (Bukhari).
Katika Imani ya kiislamu kushuhudia kuwa Mtume Muhammad ni Mjumbe wa M/Mungu na
kufuata aliyoyaelekeza kupitia suna yake ndio shahada ya pili.
Pia kutoka kwa Abu Hurairah (r.a) amesimulia kuwa Mtume (S.A.W)
aliulizwa juu ya mambo yatayopelekea watu wengi kuingia peponi, akajibu Mtume “Uchaji
mungu na tabia njema.” Kisha akaulizwa tena ni mambo yepi yatakayompelekea
mtu kuingizwa motoni? Alijibu Mtume (s.a.w) “Mdomo na tupu (viungo vya siri)”
(Tilmidhy).
Hivyo muumini wa kweli hana budi kujipamba na vipengele vya tabia
njema vilivyoainishwa katika Qur-ani na Sunna ili iwe rahisi kuipata shahada
mwisho wa maisha yake hapa ulimwenguni.
1.1 Miongoni mwa
tabia na mwenendo mwema unaosabisha mja kuipata shahada mwisho wa maisha yake.
Kujielimisha kwa ajili ya Allah. Ni katika vipengele vya tabia
njema ambayo mja humfanya kuipata shahada mwisho wa maisha yake. Kwa kupitia
tamthilia ya “Shahada” Salami mwanzo kabisa wa tamthilia anatuonesha kuwa yeye
ameshikamana na maisha ya kheri (kwamba ameshudia ya kuwa hakuna mola apasaye
kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah na kuwa Muhammad ni Mjumbe wa Allah) na
kupitia maisha hayo yanaashiria mwisho mwema wa maisha yake. Salami anatuonesha
kuwa ni mtambuzi wa mambo katika maisha yake. Na bila ya shaka alijielimisha
kwa ajili ya Allah. Hapa tunaona Salami alimsitiri muislamu mwenziwe alipopata
ajali na kufariki dunia. Alishiriki kikamilifu katika kumuosha na hatimae
kumzika. Bila ya elimu matendo haya asingeweza kuyatenda. Elimu ndio zana
aliyotunukiwa mwanaadamu ili aitumie kutekeleza majukumu yake hapa ulimwenguni.
Kama Qur-ani inavyosema. “Je wanaweza kuwa sawa wale wanaojua na wale
wasiojua?” wanaotanabahi ni wale wenye akili tu.” (39:9) Na ni hakika sio
sawa baina ya Salami na wale waliokimbia na gari baada ya kumgonga muislamu
mwenzao na kusababisha kifo chake bila ya kujali.
Kuwa na hekima. Hekima ni katika vipengele vya tabia njema
vilivyoazizi anavyotakiwa avipiganie muumini ili awe na hadhi inayostahiki na
ili aipate shahada mwisho wa maisha yake. Qur-an (2:269) “Allah humpa hekma
amtakaye na aliyepewa hekma bila ya shaka amepewa kheri nyingi. Na hawakumbuki
ila wenye akili.” Hiki ni kipengele chengine cha tabia njema kama
kinavyooneshwa katika tamthilia ya “Shahada”. Na hapa tunaoneshwa kupitia muhusika
Samira alipokuwa akimkumbusha Salami maovu yaliyofanywa na mumewe Zuberi kwa
kusema “Si unajua alivyo kisirani, si unakumbuka jana alivyokuwa akikufanya.
Yani hivi vitendo havipaendezewi kabisa kibinaadamu.
Na Nilivyoumia! Sana.” Salami alionesha wingi wa hekima kwa kutoa maneno ya hekima
na msamaha na kutaka aombewe dua ili ajuwe anachokifanya kwani hayo aliyoyafanya
kwa kutokujua kwa kusema “ Basi tumsamehe tu kwa sababu yeye hajui atendalo
tunachotakiwa kumuombea dua na mungu amsaidie na sio vizuri tena kumuongelea” .
Kadhalika Ikhalas ni katika vipengele vya tabia njema inayoweza
kusababishia mtu kuipata shahada mwisho wa maisha yake. Ikhlasi ni kufanya kila
jambo jema kwa ajili ya Allah tu. Yaani kutoa huduma na mali kwa watu wanaohitaji
msaada bila ya kutarajia malipo yoyote kutoka kwao ila kutoka kwa Allah (s.w)
Kwa Mfano kumlisha na kumvisha fukara, masikini au yatima bila ya kutarajia
hata kupata shukurani kutoka kwake ila tu kwa kutegemea malipo kutoka kwa
Allah. Qur-an (76:8-10) “Na huwalisha chakula masikini na yatima na wafungwa
na hali ya kuwa wenyewe wanakipenda chakula hicho. Husema moyoni mwao
wanapowapa chakula hicho tunakulisheni kwa ajili a kutaka radhi ya M/Mungu tu.
Hatutaki kwenu malipo wala shukurani. Hakika sisi tunamuogopa mola wetu hiyo
siku yenye shida na tabu” Hali hii inajitokeza pale ambapo Bibi kipofu na
mwanawe walipokwenda kwa Tajiri Zuberi
kuomba msaada. Zuberi kwa kiburi na jeuri na hata kuwapiga alikataa kuwapa
msaada walioutaka. Lakini Salami alionesha wingi wa ikhlas kwa kuwasaidia watu
hawa bila ya kutarajia malipo kutoka kwao kwa kuwa alikiri kuwa hapana mola
apasae kuabudiwa kwa haki ila Allah na Mtume (S.W.A) ni mjumbe wake.
Kujiepusha na riya na kujiona. Pia ni kipengele cha tabia njema
ambacho humfanya mja kuipata shahada mwisho wa maisha. Riya ni kinyume cha
ikhlasi. Kufanya riya ni kufanya jambo jema ili watu wakuone wakusifu wakupe shukurani.
Mtu anaefanya riya hafanyi wema kwa kutarajia malipo kutoka kwa Allah (s.w)
bali hufanya kwa kutarajia malipo ya hapa duniani tu iwe ni mali, sifa au shukurani.
Haya tunayapata pale Salami alipomlipia Kifimbo alipokuwa akidaiwa na
kushurutishwa kulilipa deni wanaomdai bila ya kuwa na uwezo wa kulilipa. Salami
aliyafanya haya bila ya kutaraji sifa au shukurani ila ni kutaraji malipo
kutoka kwa Allah. Qur-ani (11:15-16) M/Mungu anasema “Wanaotaka maisha ya
dunia na makombo yake, tutawapa huku duniani (ujira wa) vitendo vyao kamili
humu wao hawatapunjwa. Hao ndio ambao hawatakuwa na kitu katika akhera ila moto
na wataruka patupu walioyafanya katika dunia hii na yatakuwa bure waliyokuwa
wakiyatenda.
Kujiepusha na zinaa na tabia za kizinifu. Hiki pia ni kipengele cha
tabia njema ambacho bila ya shaka mja akidumu nacho huwa ni sababu kwake
kuipata shahada. Waumini wa kweli waliofuzu hujihifadhi na zinaa au kujiepusha
kufanya jimai nje ya mipaka iliyowekwa na Allah (s.w). Muumini wa kweli
aliyekiri kuwa hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Allah na Mtume ni
Mjumbe wake hutekeleza bila ya kusita ile amri ya Allah (s.w) ya katazo la “ Wala
usiikaribie zinaa kwa hakika huo ni uchafu na ni njia mbaya kabisa .
(17:32). Katazo hili alilitekeleza Salami katika tamthilia ya “Shahada” na
nikutokana na hilo ndio ikawa chanzo cha kifo chake na alikufa akiitoa shahada
kwamba ameshuhudia kuwa hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Allah na
Mtume ni Mjumbe wake. Mbali na vishawishi vya Samira mke wa mwajiri wake
kumlazimisha kutembea nae lakini Salami alikuwa na msimamo na kukataa katakata.
Matendo haya mema na mwenendo wa muhusika Salami ndio yaliyosababisha Salami
kufa kifo chema cha kuitamka shahada. Hivyo ni kweli kwamba kuipata shahada
kunategemea na maisha anayoishi mja.
1.2 Matendo mabaya na maovu yanayosababisha mja kukosa shahada
wakati wa kifo chake.
Kinyume chake kwa matendo maovu na mwenendo mbaya ni sababu kubwa
kwa mja kushindwa kuitamka shahada mwisho wa maisha yake hapa ulimwenguni. Na
ushahidi kamili tunaupata mwisho Zuberi alijutia yote aliyoyafanya na kushidwa
kuipata shahada wakati wa mauti yake yalipomfikia. Miongoni mwa matendo hayo
maovu yaliyomkosesha shahada Zuberi na wenzake kama Kifimbo ni kama yafutayo:-
Dharau. Hiki ni kipengele kimoja wapo cha mwenendo mbaya ambacho
huweza kumuepusha mja kuitamka shahada mwisho wa maisha yake. Mwenye kuwadharau
wengine hujihisi kuwa yeye bora kuliko mwengine. Hili ni kosa kubwa kwani
anayejua aliye mbora ni Allah (s.w) Pekee kama tunavyojifunza katia Qur-an. “Enyi
watu! Kwa hakika tumekuumbeni (nyote) kutoka kwa (yule) mwanaume ; Adam na yule
mwanamke (mmoja; Hawwa). Na tumekufanye mataifa na makabila (mbali mbali) ili
mjuane. Hakika ahishimiwaye sana miongoni mwenu mbele ya M/Mungu ni yule
amchaye Mungu Zaidi katika nyinyi…” (49:13). Tajiri Zuberi alimdharau sana
Salami, alimuona mjinga sana hata kumwita “Bwege nazi mkubwa”, “Kelbu mkubwa”,
“Mshenzi wewe” “Shuwaini”, Kenge maji”, “Punda”. Haya na mengine ndio yaliyomsababisha
Tajiri Zuberi kuikosa shahada wakati wa kifo chake.
Tabia ya matusi na maneno machafu. Pia ni
mwenendo mbaya ambao bila ya shaka huweza kumzuia mja wakati wa kutoka roho
yake kuitamka shahada. Tajiri Zuberi alikuwa na matusi na maneno machafu katika
kinywa chake kwa lengo la kumdhalilisha Salami. Kwa waislamu kuna katazo kubwa
juu ya hilo. Tumekatazwa kutukanana na hata kuitana majina tusiyoyapenda kwa
kejeli. M/mungu katika Qur-an anasema “…Wala msitukanane kwa kabila wala
msiitane majina mabaya (ya kejeli). Jina baya kabisa kuitwa mtu ni “Fasiq”
baada ya kuwa yeye ni muislamu. Na wasio tubu basi hao ndio madhalimu. (49:11).
Tukirejea mafundisho ya Mtume tunayapata kupitia hadithi kutoka kwa Abu Hurairah (r.a) amesimulia kuwa Mtume (S.A.W)
aliulizwa juu ya mambo yatayopelekea watu wengi kuingia peponi, akajibu Mtume “Uchaji
mungu na tabia njema.” Kisha akaulizwa tena ni mambo yepi yatakayompelekea
mtu kuingizwa motoni? Alijibu Mtume “Mdomo na tupu (viungo vya siri)”
(Tilmidhy). Kwa hiyo jambo moja kubwa alilokuwa nalo Tajiri Zuberi ni Mdomo
mchafu na huu ndio uliomkosesha kuitamka shahada wakati wa kifo chake.
Kadhalika kutokuwa na huruma. Ni miongoni mwa mwenendo mbaya ambao
humzuia mja kuikosa shahada mwisho wa maisha yake. Tajiri Zuberi alijipamba na
mwenendo huu ovu wa kutokuwa na huruma. Aliwashambulia masikini waliokuwa na
mahitaji kwa jeuri na kiburi na mwisho kuwafukuza bila ya huruma kwake na haya
ndio yalikuwa maneno yake walipokuwa wakijibizana na masikini waliokuja kutaka
msaada. “ Kwanza nani aliyewatuma mje hapa? Hivi mimi naweza kuzaa mjusi kama
wewe! Nakuuliza naweza kuzaa mjusi kama wewe? Na wewe mama kipofu umepita
majumba yote huko hukuona pakuingia isipokuwa huku eh! Nikusaidie nini? Toka
hebu kwenda huko na wee mama nenda huko pumbavu! Kwendeni!”
Muunini wa kweli hana budi kujipamba na tabia ya kuhurumia
viumbe wenzake. Amuonee huruma kila
mwenye shida na ajitahidi kumsaidia inavyowezekana. Katika kuonesha umuhimu wa
kipengele hiki katika uislamu Mtume (s.a.w) amesema “Ambaye hahurumii watu,
pia Allah (s.w) hatamhurumia” (Bukhari). Huruma hudhihiri katika kuwasaidia
wenye shida na matatizo kwa mali na kauli kama Qur-ani inavyotufunza “
Hamtaweza kufikia wema mpaka mtoe katika vitu mnavyovipenda na chochote
mnachokitoa, basi hakika Allah anakijua”. (3:92). Tabia hii mbaya ya
kutokuwa na huruma kwa wenye shida ndio moja miongoni mwa nyingi zilizomponza Tajiri
Zuberi kuikosa shahada wakati wa kifo chake.
Unafiki ni miongoni mwa tabia mbaya na ovu kwa muumini. Mnafiki ni
yule anaekubali uislamu mdomoni (kwa kauli tu) lakini moyoni mwake na katika
matendo yake anaukanusha. Kupitia Qur-an (2:8-9). “ Na katika watu wako
wasemao tumemuamini M/Mungu na siku ya mwisho hali ya kuwa wao si wenye
kuamini. Wanataka kumdanganya Allah na wale walioamini, lakini hawadanganyi ila
nafsi zao, nao hawatambui”. Kifimbo kaonesha unafiki pale anapokuja kwa
Salami muislamu mwenziwe ni mtu mwema wakati huo huo akenda kazini kwake
anamchongea kwa mwajiri wake. Na akirudi
tena kwa Salami humchonganisha yeye na mkewe, na hatima yake mke wa Salami
kuomba talaka kwa mumewe kwa unafiki wa Kifimbo kusema kuwa Salami ana mke
mwengine. Matendo haya ya Kifimbo ni ya kinafiki na ni matendo maovu ambayo
yanaweza kuwa sababu kwa mja kuikosa shahada mwisho wa maisha yake.
Kiburi na majivuno. Kiburi, majivuno na majigambo ni katika tabia
mbaya iliyokemewa vikali katika Qur-an kama ifuatavyo (31:18). “Wala
usiwatazame (watu) kwa upande mmoja wa uso, wala usiende katika ardhi kwa
maringo, hakika Allah hampendi kila ajivunae ajifaharishaye” Zuberi anajiona
kuwa ni bora kwa Salami na ni wajuu na wa maana zaidi kuliko Salami. Kiburi
hicho na kujiona kulisababishwa na neema (utajiri) aliotunukiwa na mola wake. Tabia
hii ovu ndio iliyokuwa sababu kwa tajiri Zuberi kujuta na kuikosa shahada
wakati kifo kilipomfikia.
Kuikimbilia zinaa na tabia za kizinifu. Ni miongoni mwa tabia mbaya
ambayo ni moja kati ya zile zinazoweza kumzuia mja kuipata shahada mwisho wa
maisha yake. Katika tamthilia ya “Shahada” tumeoneshwa Samira (mke wa tajiri
Zuberi) ni mwenye kuikimbilia zinaa na ni mwenye tabia za kizinifu. Samira alifanya
kila analoweza kumrubuni Salami atekeleze matamanio yake anayotaka. Alimpa pesa
sio kwa kumsaidia bali kwa lengo la kumhonga. Hatima yake alimfungia milango
kwa kumlazimisha afanye nae zinaa japo kwa mara moja tu. Na jambo hili ndio
sababu kwa mumewe kumteka Salami na kumuadhibu. Na pia ndio sababu kupoteza
maisha yake bila ya kuipata shahada. Mwenendo huu na tabia hii ya uzinifu sio
tabia njema kwa muumini aliyeshuhudia kuwa hakuna mola apasaye kuabudiwa kwa
haki isipokuwa Allah na kuwa Muhammad ni Mjumbe wa Allah.
2.0 Hitimisho
Kupitia tamthilia ya “Shahada” ni dhahiri kwamba kuipata shahada
mwisho wa maisha ya mja duniani kunategemea na jinsi anavyoendesha mja maisha
yake. Haya yanathibitika kupitia muhusika Salami ambapo maisha yake yote
aliishi kwa kujipamba na tabia njema na kutennda yaliyo mema kama vile
kujielimisha kwa ajili ya Allah kwa kutenda matendo mema kwa ujuzi na elimu
sahihi, kuwa na hekima, kuwa na ikhlasi, kujiepusha n aria, na kujikinga na
zinaa. Na kinyume chake kuikosa shahada kunategemea na mwenendo wake hapa
ulimwenguni. Haya tunaoneshwa na Tajiri Zuberi katika tamthilia ya “Shahada”
pale alipojipamba na tabia mbaya na mwenendo mbaya kama vile; kuwa nadharau,
kuwa na tabia ya matusi na maneno machafu, kutokuwa na huruma, na kuwa na
kiburi na majivuno ya kupindukia. Haya na mengineyo ndio sababu kwake kuikosa
shahada mwisho wa maisha yake.
MAREJEO
Al-farsy, A. S (1993).Qur-an Takatifu, The Islamic
Foundation. Nairobi Kenya.
An-Nawawi, Y. S (2009). Matnu Arbain Nawiyyah na Tafsiri yake.
Ibn Hazm Media Center. Dar-es-salaam. Tanzania.
IPC. (2003). Nguzo za Uislamu, Darasa la Watu Wazima Juzuu ya 2.
Islamic Propagation Centre DSM. Tanzania.