Tuesday, February 2, 2016

HATUA ZA KUFASIRI MATINI.


HATUA ZA KUFASIRI MATINI ZA AINA MBALI MBALI.
Mwansoko na wenzake (2006) Tafsiri ni zoezi la uhawilishaji (Transferring) wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.

Merinyo, F. A (2014) akimnukuu Mshindo (2010:2) anasema kufasiri ni kufafanua maana ya matini moja na kutayarisha baadae matini nyengine inayowiyana nayo ambayo huitwa tafsiri na ambayo inawakilisha ujumbe ule ule uliomo katika matini ya awali kwa kutumia lugha nyengine.

Wataalamu mbali mbali wameainisha hatua kadhaa za kufuatwa katika mwenendo mzima wa kufasiri matini mbali mbali. Katika kujadili swali hili tutajadili hatua saba (7) kama zilivyoainshwa na Mwansoko na wenziwe  (2006). Hatua hizo ni kama ifuatavyo:

Hatua ya maandalizi, uchambuzi, uhawilishaji, rasimu ya kwanza, udurusu wa rasimu ya kwanza, kusomwa kwa rasimu na mtu mwengine na usawidi wa rasimu mwisho.


Hatua ya kwanza ni hatua ya maandalizi. Hatua hii inahusisha mambo matatu ambayo ni  Kupitia sehemu muhimu za matini chanzi, kwa mfano; istilahi, majina ya wahusika, majina ya kijiografia, maeneo au kauli zisizofasirika kirahisi. Kupata marejeleo ili kutafuta visawe vya kisemantiki. Kutafuta na kuandika visawe hivyo. Kadhalika hatua hii mfasiri huchunguza taarifa zinazohusu usuli wa matini chanzi. Hizi ni taarifa zinazohusu mwandishi wa matini, mazingira ya uandishi wa matini chanzi, malengo yake, utamaduni wa wazungumzaji wa matini chanzi na hadhira lengwa ya matini chanzi. Katika kuudurusu usuli wa matini chanzi mfasiri pia anapaswa kuzingatia sifa za kiisimu za matini anayotaka kuifasiri. Wakati huo huo mfasiri huandika pembeni (kwenye daftari maalumu) misamiati na istilahi muhimu maneno ya kitamaduni na sehemu ngumu katika matini chanzi ambazo zinahitaji uchunguzi na utafiti zaidi. 

Hatua ya pili ni uchambuzi. Katika hatua hii mfasiri huchunguza kwa makini maneno pamoja na maelezo muhimu ya matini chanzi aliyoyaandaa katika maandalizi ili aweze kuyatafutia visawe stahili katika lugha lengwa. Zoezi la uchambuzi hufanywa kwa kutumia marejeo mbali mbali, kama vile kamusi. Inashauriwa kuwa mfasiri awe na buku na notisi au faili kwa ajili ya kuandika na kuhifadhi maneno na maelezo muhimu na visawe vya matini chanzi. Visawe vilivyokubalika viorodheshwe vizuri ili iwe rahisi kurejelewa wakati wa kufasiri. Ikiwa matini chanzi ni kubwa sana mfasiri huwa hana budi ila ni kuigawa katika sehemu ndogo ndogo kama sura, aya na sentensi na kuitafasiri sehemu moja baada ya nyengine. Hata hivyo inashauriwa kwa mfasiri kwamba aya iwe ndio kizio cha msingi katika tendo la kufasiri.     


Hatua ya tatu baada ya maandalizi ni uhawilishaji (transferring/transference). Katika hatua hii mfasiri huhawilisha ile taarifa kutoka kwenye matini chanzi kwenda kwenye matini lengwa, hapa mfasiri anatakiwa kuzingatia sarufi ya lugha lengwa na lugha chanzi. mfano; “My new house is broken”-Yangu jipya nyumba ni vunjika. Tafsiri ya Kiswahili fasaha inapaswa kuwa “Nyumba yangu mpya imebomoka” Uhawilishaji maana yake ni kuhamisha maana, ujumbe nk. kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa kwa kuzingatia sarufi ya lugha lengwa, lengo la matini au mwandishi, umbo la matini, mtindo nk.
Mbinu ya tafsiri ambayo inatumika katika hatua hii ya uhawilishaji ni tafsiri ya neno kwa neno.


Kadhalika hatua ya nne ni kusawidi rasimu ya kwanza (drafting). Uhawilishaji wa visawe kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa unapokamilika kinachopatikana ni rasimu ya kwanza ya tafsiri. Rasimu ni kitendo cha kuandika matini au Makala yoyote kwa mara ya kwanza kwa mujibu wa utaratibu BAKIZA (2010). Mfasiri anapoanza kusawidi rasimu ya kwanza ya tafsiri yake atashuhudia kuwa anahitaji taarifa au ufafanuzi zaidi kuhusu uchambuzi aliokwishafanya mwanzo. Kwa hivyo atalazimika kufanya uchunguzi zaidi usuli wa matini na hata kupekuwa tena kamusi na marejeo mengine aliyotumia. Pia anapofanya uhawilishaji wa maana, mfasiri inafaa azingatie umbo la matini chanzi kuhakikisha kuwa linaakisiwa na matini lengwa. Mfano iwapo matini chanzi ni shairi la tathlitha (mistari mitatu) sura au umbo hilo halina budi kurudiwa katika matini lengwa. Akiwa nasawidi rasimu ya kwanza mfasiri inafaa afikirie hadhira anayoilenga pamoja na lengo la matini chanzi, kwani mambo haya huathiri mno usawidi wa tafsiri. Rasimu ya kwanza ya tafsiri inakuwa na dosari nyingi na kwa hiyo haifai kupelekwa kwa mteja au hadhira. Badala yake rasimu ya kwanza lazima ipitiwe tena na kurekebishwa au kudurusiwa.


Vile vile hatua ya tano ni kudurusu rasimu ya kwanza ili kuunda rasimu ya pili. Mfasiri hupata fursa ya kwanza ya kuitathimini na kuifanyia marekebisho tafsiri yake mwenyewe. Kazi ya kudurusu haipaswi kufanywa haraka. Wataalam wengine kama vile Larson (1984) anasema rasimu ya kwanza ni lazima iachwe kwa muda wa wiki moja. Udurusu unahusisha shughuli zifuatazo:
Kusahihisha makosa ya kisarufi, miundo isiyoeleweka vizuri.

Kunyoosha sehemu zenye tafsiri ya mzunguko na zenye matumizi potofu ya visawe. Mfano; “They rarely visit me these days – Siku hizi ni aghalabu-nadra sana wao kunitembelea.” Kurekebisha sehemu zenye muunganiko tenge au mbaya ambazo zinazuia mtiririko mzuri wa matini. Kuhakiki usahihi na kukubalika kwa maana zinazowasilishwa katika matini lengwa. Hapa tunaangalia kama kuna mambo yameongezwa, yamepunguzwa au yamepotoshwa/kubadilishwa. Kuhakiki kukubalika kwa lugha uliyotumia katika tafsiri yako kwa kuzingatia umbo na mada ya matini chanzi.
Kuona iwapo mada au ujumbe mkuu wa matini chanzi unajitokeza waziwazi katika matini lengwa.

Baada ya kuzingatia masahihisho hayo mfasiri atalazimika kutoa rasimu yake ya pili ambayo inashauriwa ampe msomaji mwengine ili aidurusu na kupendekeza masahihisho zaidi. Jambo hili litasababisha kwenda hatua nyengine inayofuata katika mwenendo wa kufasiri.

Kwa kuendelea hatua ya sita  ni kusomwa rasimu ya pili na mtu mwingine. Msomaji wa rasimu ya pili anaweza kuwa mfasiri au shabiki wa tafsiri, mhakiki au mhariri wa tafsiri, anaweza kuwa mpenzi wa tafsiri mbali mbali au mtu mwingine yeyote anayemwamini mfasiri. Katika hatua hii mfasiri anashauriwa atumie mbinu zifuatazo katika kumpata mtu mwengine ili kuisoma tena rasimu ya pili Kumpa bila kumjulisha kwamba ni tafsiri kumpa matini chanzi na matini lengwa ili alinganishe. Inapendekezwa kwamba mtu huyo asome kwa sauti ili uweze kubaini upungufu na iwapo atafikia pahala na kusita katika usomaji wake basi uwezekano mkubwa wa sehemu hizo za matini kuwa zina matatizo ya kiufasiri matatizo hayo yanaweza kuwa ni matumizi potofu ya viunganishi vya sentensi, upotoshaji wa maana za maneno, uendelezaji mbaya wa maumbo ya maneno au mikanganyiko katika matumizi ya mitindo. Hali hii ikitokea mtu aliyepewa kuidurusu rasimu ya pili atalazimika kuweka alama maalumu sehemu zenye matatizo na kisha kumuelekeza mfasiri azichunguze tena na kuzirekebisha.


Na mwisho ni hatua ya saba nayo ni kusawidi rasimu ya mwisho. Katika hatua hii mfasiri atafanyiakazi maoni na mapendekezo ya msomaji ambaye alimpa kazi yake. Matokeo ya kufanyiakazi maoni husababisha kupatikana kwa rasimu ya mwisho ambayo ndiyo humfikia mteja, hadhira, wachapaji na wengineo wanaolengwa iwafikie.

Hizi ndizo hatua zinazofaa kufuatwa katika mwenendo wa kufasiri matini za aina mbali mbali. Hata hivyo katika mwenendo halisi wa kufasiri inawezekana hatua hizi zisifuatwe katika mpangilio ulielezwa hapo juu. Hii ni kwa kuwa na ukweli kwamba wakati wa tendo la kufasiri mfasiri hulazimika daima kwenda mbele na nyuma kutoka katika matini chanzi mpaka kwenye matini lengwa. Pamoja na hayo ni muhimu kwa mfasiri kutambua kuwa kuna hatua zilizotajwa hapo juu katika mwenendo mzima wa kufasiri matini mbali mbali ambazo ni vyema kuzifuata kila inapowezekana.
 

MAREJEO.

Merinyo, F. A (2014). Tafsiri na Ukalimani (Utangulizi Muhimu katika Tafsiri

                               na Ukalimani). Mkuu-Rombo. Tanzania.

Cartford, J. C. (1965). A Linguistic Theory of Translation. London: OUP.
Larson, L. M. (1984). Meaning-based Translation. London: University Press

                               of America.
Mwansoko, H. J. M. na wenzake (2006). Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na

                                                         Mbinu. Dar es Salaam: TUKI

BAKIZA (2010). Kamusi la Kiswahili Fasaha. OUP. Nairobi Kenya.