Kukua
au kuimarika na kufifia au kufa kwa Sanaa za maonyesho.
(Jando,
Unyago na Michezo ya watoto)
1.
Utangulizi
Sanaa
za maonyesho zimekusanya vipengele mbali mbali, vipengele hivyo ni kama:- Sherehe mbali mbali (harusi,
siasa), ngoma mabali mbali, masimulizi
ya hadithi, kusalia miungu, majigambo, ngonjera, tamthilia, michezo ya watoto, jando,
unyago, utani na nyenginezo. Vipengele hivyo kila kimoja kinamaana
inayojipambanua na kipengelele chengine katika utendaji wake. Kadhalika sanaa
za maonyesho namna zilivyokuwa zikitekelezwa zamani ni tafauti na zinavyotendwa
sasa. Hali hii ya utendaji hubadilika kulingana na nyakati, husababishwa na
mambo mbali kama vile maendeleo ya sayansi na teknolojia, dini, mitazomo ya
watendaji (fanani na hadhira) na hata hali ya mabadiliko ya mazingira katika
jamii zinazohusika. Sanaa za maonyesho au tendaji hutendwa kwa namna mbali
mbali kulingana na jamii inayohusika.
Tanzania ikiwemo Zanzibar sanaa hizi za maonyesho hutendwa au
hutekelezwa kwa namna tafauti na jamii nyengine nje ya Tanzania. Katika Makala haya tutajadili na kufafanua
namna Sanaa za maonyesho (Jando, Unyago na Michezo ya watoto) zilivyoshamiri
hapo mwanzo na namna zinavyofifia au kufa kwa sababu mbali mbali.
2.1
Maana ya sanaa za maonyesho. (Jando, Unyago na Michezo ya watoto)
Sanaa
za maonyesho ni sanaa kongwe na muhimu katika fasihi simulizi. Kipera hichi
kimeelezwa na wataalamu mbali mbali na kubainisha mambo muhimu yanayozibainisha
katika utendaji wake. Wataalamu hao ni kama Semzaba, E (1997:1) Sanaa za
maonyesho ni uonyeshi wa maisha kisanii ambapo mwonyeshaji na hadhira huwepo
mahali pamoja na wakati mmoja. Katika fasili hii inabainika kuwa sanaa za
maonyesho ni namna ya kuonyesha maisha kisanii ambapo mwonyeshaji na anaeonyeshwa
huwa mahali pamoja kwa wakati mmoja katika tendo la uonyeshi huo. Kipera hiki
pia kimeelezwa na kuwekwa bayana na Mulokozi, M (1996:187) Sanaa za maonyesho
ni tukio au tendo la kijamii lenye sifa zifuatazo:- Dhana inayotendeka, uwanja
wa kutendea, watendaji, hadhira, kusudio la kisanaa, muktadha wa kisanaa na
ubunifu. Katika fasili hii Mulokozi anabainisha sifa za sanaa za maonyesho
kwamba Sanaa za maonyesho haziwezi kuwa na kuitwa sanaa za maonyesho hadi ziwe
na sifa mahsusi ambazo zinazipambanua na vipera vengine vya fasihi simulizi.
Wataalamu wengine hawakuwa nyuma katika kufafanua Sanaa za maonyesho wakiwa na
maana inayolingana na wataalamu Semzaba na Mulokozi. Miongoni mwao ni kama
Fulgence, L. Mbunda (1996) yeye anasema kuwa “Sanaa za maonyesho ni mchezo,
matendo mbali mbali mathalan ya waganga na maigizo juu ya vita, harusi au
wakati wa ngoma. Mhando na Balisidia (1976:2) Sanaa za maonyesho ni kitendo
chochote chenye sifa nne ambazo ni mchezo, mchezaji, uwanja wa kuchezea na
watazamaji. Dhana ya sanaa za maonyesho ni kongwe katika jamii za kiafrika
ikiwemo Tanzania. Kwa
mujibu wa http://www.chomboz.blogspot.com. “Sanaa za maonyesho za asili yaani
za jamii ambayo utamaduni wake ulikuwa haujaingiliwa na wakoloni (wageni)
kugawanywa katika makundi matano mbazo ni (i) sherehe (ii) ngoma (iii)
masimulizi ya hadithi (iv) kusalia miungu (v) majigambo.” Ingawa zipo aina
nyengine za sanaa za maonyesho kama ngonjera, tamthilia, michezo ya watoto,
jando, unyago, utani na nyenginezo zinaingia katika kundi la Sanaa za maonyesho
kwa umbon lake la utendaji wa matendo ya dhati na yale ya kisanaa. Nukuu hii
inatubainishia vipengele mbali mbali vilivyomo katika kipera hichi kama
vilivyotajwa hapo juu. Miongoni mwao ni jando, unyago na michezo ya watoto.
2.2
Maana ya Jando
Kamusi la Kiswahili Fasaha
(2010:129) linasema kwamba Jando ni
pahali wanapowekwa watoto wa kiume wanapotahiriwa= chari au ni tendo la
kumtahiri mtoto wa kiume.
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili
Sanifu (2004:128). Inaeleza Jando “ kumdi
la wototo wanaume wanapotahiriwa na kufundishwa mambo ya utu uzima.” Fasili
hii inatubainishia kwamba jamii nyingi duniani wanapowataarisha watoto wao wa
kiume kuingia ukubwani huwapa mafunzo yatakayoweza kuwaongoza katika kipindi
chote chao cha utuuzima. Pia katika kitendo hicho watoto wakiume hutahiriwa ili
kukaribishwa ukubwani.
Haji A. I na wenzake (1981:75)
wanatubainishia dhana hii ya Jando
kwa kusema “Katika sehemu hii, kutokana na mila za jamii, watu huwa
wanatambulishwa rasmi mabadiliko hayo. Mfano ngoma za jadi jando na unyago zimo
katika jamii za Kiafrika. Ambapo jando kwa kawaida ilikuwa kwa wale wavulana
ambao wameshakuwa wakubwa kiasi ambacho wanataka waelezwe majukumu yao kuhusu
namna ya kuishi katika jamii kwa marika hayo waliyofikia. Umri hutafautiana
kati ya jamii na jamii. Kwenye shughuli yenyewe huweko matendo ambayo ni
maigizo ya mafunzo hayo wanayotakiwa wayapate.” Nukuu hii inatueleza maana
halisi na matendo yanayofanyika katika jando kwa watoto wa kiume.
2.3
Maana ya Unyago.
Kwa mujibu wa Kamusi la Kiswahili
Fasaha (2010:432) linaeleza kwamba Unyago
ni mafunzo wanayopewa wasichana ya mila za jamii yao au ni ngoma ya
vielelezo inayochezwa katika mafunzo hayo.
Pia Kamusi la Kiswahili Sanifu (2004:436).
Linaeleza Unyago “ mkusanyiko wa
vijana mahali maalumu ili kufundishwa mila za kabila au ngoma ya kuwafundisha
wari mila za kabila lao.” Fasili hii inatuarifu kwamba kwa upande wa watoto wa
kike tendo la kuwapa mafunzo ili waingie katika utuuzima huitwa Unyago.
Kadhalika wataalamu Haji, A. I na
wenzake (1981:75) kwa kusema “Unyago kwa kawaida huchezewa wasichana ambao
wamekwisha vunja ungo. Nao pia inakuwa ni sherehe ya kujua kwamba msichana
fulani ameshatoka katika kundi la watoto na sasa yumo katika kundi la watu wazima.
Humo huwemo mafunzo ambayo ndiyo yanayotakiwa katika jamii ili yaendelezwe au
ayafanye huyo anayefikia umri huo.” Kwa hivyo maelezo hayo yanatafautisha baina
ya Jando na Unyago kwamba ni sherehe za kuwafunza watoto wa kike na kiume
wanapoingia katika kundi la watu wazima.
2.4
Ufafanuzi zaidi kuhusu Jando na Unyago.
Kwa mujibu wa Kayombo, F (2014)
katika blogsport yake ya kijamii anaeleza kwamba “ Jando na Unyago ilikuwa
ni shule ya malezi bora kwa vijana ambao walikuwa wanahama toka rika ya watoto
kuwa watu wazima.
Mafunzo ya jando kwa wavulana
yaliendana na kutahiriwa na hata kwa wasichana katika baadhi ya makabila.
Makabila maarufu katika utamaduni huu ni Wazaramo,Wamakonde, Wakrya, Wayao na
makabila mengi ya mkoa wa Singida. Vijana waliwapatiwa mafunzo juu ya maadili
bora, kuwaheshimu wakubwa, kuwa shupavu, uwajibikaji, majukumu ya kuilinda
familia, ukoo na kabila.
Mafunzo ya Maisha kwa Vijana
Kupitia Jando na Unyago. Mafunzo katika jando na unyago yalikuwa na nia ya
kumuandaa kijana kuingia katika majukumu ya utu uzima. Wasichana walifundishwa
jinsi ya kutunza nyumba, jinsi ya kutunza watoto, lakini pia lazima tuseme
walifundishwa jinsi ya kufanya mapenzi na kumridhisha mume.” Bila ya shaka kwa vile Zanzibar ni visiwa
basi watu wake wanamchanganyiko changamano wa watu wenye asili mbali mbali
yakiwemo makabila yaliyotajwa hapo juu na Bw. Kayombo, F (2014) katika mtandao wake wa kijamii.
2.5
Maana ya michezo ya watoto.
Michezo ya watoto. Kwa mujibu
wa Haji, A. I na wenzake (1981:75) “
Shughuli ya kutawazishwa mkuu wa mji (chifu) shughuli za uganga, kusalia miungu
na michezo mingi ya watoto kama bui, ngodani n.k pia ni aina za sanaa za
maonyesho.” Katika nukuu hii inabainika
kuwa michezo ya watoto ni miongoni mwa Sanaa za maonyesho.
Dhana ya michezo ya watoto
imajadiliwa pia na mtaalamu Haji, M. O. (2010:51). Michezo ya watoto ni michezo
ambayo watoto wanacheza katika mazingira yao wanamoishi. Watoto hufanya hivyo
kutokana na kuiga mambo ambayo wanayaona katika jamii wanayoishi. Kwa mfano
watoto wanaweza kucheza mchezo wa Kinyuli, Kachiri, Chura mwanamatumbatu,
Matango manemane n.k. Michezo hii yote huchezwa hapa petu Tanzania bara na
Visiwani. Watoto wanapocheza michezo yao katika jamii huwapatia faida nyingi
sana kama vile:-
kuimarika viungo vyao vya mwili
kwani katika kucheza watoto huweza kukimbia au kutenda mambo mbali mbali ambayo
husaidia kuimarisha viungo vya mwili, wakati huo pia hujipatia burudani
inayoambatana na fasihi simulizi pamoja na hayo watoto pia hupata nafasi ya
kujiona na wao kuwa ni sehemu ya jamii na wanaweza kufanya kazi ya ujasiri
katika mazingira yao.
Hata hivyo wazazi wanapowaona watoto
wanacheza vizuri hupata fursa katika nafasi zao na kujiona kuwa watoto wao wako
katika afya njema na kwa hivyo watoto hujenga urafiki au uhusiano mwema baina
ya watoto wanaocheza na wazee wao.
3.0 Kukua au kuimarika kwa Sanaa za maonyesho (
Jando, Unyago na Michezo ya watoto)
Makala haya yana lengo la
kueleza Jando, Unyago na Michezo ya watoto katika kukuwa katika
jamii za kizanzibari.
Jando na Unyago uliimarika kutokana
na kwamba wanajamii wa nyakati zilizopita waliamini kwamba ni kama chuo cha
kutoa mafunzo mbali mbali kwa vijana wa kike na kiume.
Mzee Suleiman Abdalla Suleiman
anasema:-
“ Mimi
ninavyofahamu wari hufundishwa namna ya kuishi vizuri na mume pamoja na
kumhudumia, kumtunza mume na watoto au familia kwa jumla na kijana wa
kiume barobaro hufundishwa jinsi ya
kuishi vizuri na mke.”
- Mzee Suleiman Abdalla (Zanzibar, 2015).
Kwa hivyo wanajamii wa nyakati hizo
walithamini na kutukuza harakati hizo kwa kuwa ilikuwa ni darasa tosha kwa
watoto wao na kujenga jamii yao kwa kufuata mila na desturi zao.
Michezo ya watoto pia ilikuwa ni
chuo cha watoto katika kujenga mashirikiano miongoni mwa jamii. Haya
yamethibitishwa na mtaalamu Haji, M. O. (2010:51). “ Hata hivyo wazazi
wanapowaona watoto wanacheza vizuri hupata fursa katika nafasi zao na kujiona
kuwa watoto wao wako katika afya njema na kwa hivyo watoto hujenga urafiki au
uhusiano mwema baina ya watoto wanaocheza na wazee wao.”
Kadhalika muktadha huo Bi Rahma
Abass
anatuhakikishia kwa kusema:-
“Tulikuwa
tunacheza uwanjani tukiwa watoto wa kila nyumba katika kijiji chetu Mchangani
(Shamba). Nyumba ya mlezi wangu ilikuwa na duka mbele ya duka hili palikuwa na
uwanja mkubwa ukimurikwa na karabai siku za mbaamwezi sheti kweupeee..
iliyokuwa karabai ikininginia kwenye kipenu cha gunia cha duka hili. Wazee wetu
walikuwa wamejipumzisha barazani mwa nyumba zao za udongo wakitutazama na
kuendelea na mazungumzo yao. Sisi tukicheza michezo mbali mbali na kuimba,
nakumbuka mchezo wa “Ngoda ngadani na Kitambaachangu cheupe. Aliimba:-
“
kitambaa chngu cheupe
Kinamadoa
meupe
taishi
miaka yote na dada Patima ubenduke
bendu!
na
tena ubenduke
bendu!
…….”
Kwa
kweli ilikuwa raha natamani nirudi utoto sasa yale yote hayapo yametoweka too… kwa watoto wetu wa kisasa TV zimewateka hawana muda wa kucheza
pamoja.”
- Bi Rahma Abass Madeweya (Zanzibar, 2015)
Katika maneno hayo tunaona mandhari
iliyokuwepo wakati huo na namana jamii ilivyokuwa pamoja kuwalinda na kuwalea
watoto wao kwa uangalifu uliokuwa mkubwa kabisa.
Kadhalika Jando na Unyago pamoja na
Michezo ya watoto iliaminika kuwa ni
hospitali ya uchunguzi wa maradhi pamoja na kuimarisha afya za watoto wao. Wari
walipokuwa ndani walikuwa wakichunguzwa afya zao za mwili. Mfano mwanamke
alikuwa akichunguzwa maradhi katika sehemu zao za siri mfano maradhi ya “Vikanga”
maradhi hayo walikuwa wakiangaliwa na Nyakanga na pale yanapobainika maradhi
hayo hukatwa kwa viwembe na baadae hutiwa dawa za kienyeji na kupona.
Iliaminika maradhi ya “Vikanga” ikiwa
hayakuondoshwa mapema kwa kijana wa kike anaweza kuwa tasa au akibahatika kuzaa
mtoto anatangulia (kufa). Pia kwa upande wa vijana wa kiume hupimwa urijali wao
na pindipo anapoonekana ana matatizo basi hutibiwa ili aweze kummudu vyema
mkewe atakapo oa. Kadhalika ilikuwa kwa vijana wa kiume hufanyiwa tohara
(kutahiriwa) kama Mzee Abdalla Suleiman Abdalla anasema:-
“
Ngariba huwatahiri watoto kuwakata magovi yao ya uume wao kwa kutumia visu
vidogovidogo ambavyo huwa maalumu kwa kazi hiyo tu. Walikuwa wakivishwa vishuka
shingoni. Wakati wakiwa ndani huko walikuwa wakipikiwa vyakula mbali mbali vya
asili kama vile uji wa mtama wakati wa asubuhi mpaka wakakatika jasho
chururuuu… inapofika jioni wanachinjiwa kuku na wanakula wao pamoja na Ngariba
na Nyakanga. Muda wote huo hukaa ndani hadi kupona majaraha yao.”
-Mzee Abdalla Suleiman
Abdalla(Zanzibar, 2015)
Bi Halima Zaidi Sizamani
anasema kwa upande wa wari:-
“Ah!
Mbona makubwa wajukuu wangu! haya yalikuwa siri! Tena siri kubwa hatukupaswa
kuyasema hadharani lakni …….. mimi nilivyoona wari huwekwa ndani hukoo hukaakaa huko hadi
kufunzika mafunzo ya jamii kama vile masuala heshima na urembo kwa wanawake
kama kutunga shanga na kusaga liwa na namna ya kujishughulikia wakati wa hedhi
hupewa vitambaa maalumu wakati huo waliita Mrekani (Mbinda)
na walikuwa wakifundishwa namna ya kuitengeneza na kuivaa ili kuzuia hedhi bila
ya kuonekana na kujuulikana kwamba yumo katika siku zake ”
-Bi Halima Zaidi Sizamani (Zanzibar,
2015)
Kwa
upande mwengine jando, unyago na michezo ya watoto ilitumika na kutendwa kama
ni kuendeleza mila na desturi za jamii.
Bi Halima Zaidi Sizamani anasema wakati wa majadiliano ya ana kwa ana
“ Wajukuu zangu Unyago ulikuwa ni chuo kikubwa kwa watoto waliokwisha
vunjaungo kwani walifundishwa jinsi ya kuziendeleza mila na desturi kama vile
kuepukana na kufanya machafu baada ya kuwa watu wazima, kuwa na nidhamu kwa
waliowazidi kama kupokea mzigo wa mkubwa wake anapomuona amebeba mzigo huo na
hasa mume kumpokea anapoingia ndani mwake wakiwa mume na mke.”
- Bi Halima Zaidi Si Zamani ( Zanzibar, 2015)
Kwa hivyo mila na desturi
zilisisitizwa kuendelezwa kwa wanajamii wote, na jamii ilirithisha mila na
desturi hizo kupitia jando na unyago kizazi hadi kizazi.
Mzee Suleiman Abdalla aliendelea kusema:-
“Baada
ya siku kadhaa kupita katika Jando na Unyago wakati waliotahiriwa washapona
majaraha yao na wari kumaliza mafunzo yao hutolewa nje. Siku wanapotolewa nje
ilifanywa sherehe kubwa ambayo wazazi wa watoto waliowekwa Jandoni na Unyagoni
walikuja kuwaona watoto wao wakiwa wamepona na wamefunzika pamoja na watu
wengine walihudhuria sherehe hizo pakiwa na ngoma za asili na nyimbo zikitumbuiza.
Kwa kweli ilikuwa inavutia. Sasa haya nadra kuyaona na wala hamyajui au
mnayajua? Subutuuu…”
-Mzee Suleiman Abdalla (Kwamtipura, Zanzibar 2015)
Katika maneno haya tunagundua kuwa
ngoma zilishiriki kutumbuiza wanajamii katika sherehe za jando na unyago na
ndio ilikuwa kitambulisho cha jamii inayohusika ingawa kila jamii inatumia
ngoma zao wakati wa sherehe mbali mbali. Kwa upande wa Pemba siku ya sherehe
wari walipambwa kwa kuvishwa kanga mbili na baadae hupelekwa kila nyumba na
kupiga hodi kwa majirani na kuamkia waliokuwemo na baadae hupewa zawadi kama
pesa, kanga, nguo au vitambaa na vyenginezo..
Mimi baada ya kupata ukubwa
nilipelekwa kwa Nyakanga mkubwa kwa jina maarufu la Bibi wa mbuzini” niliekwa
ndani na kufunzwa kwa muda wa siku saba. Na siku ya kutolewa ilifanywa shehere
ndani. Sherehe hii niliimbiwa nyimbo na kupigwa ngoma ya msondo.
Mfano wa nyimbo hizo ni:-
“Kwa
mume kuna ngondo hakuna kitu cha bure
Kwa
mume kuna ngondo hakuna kitu cha bure
hakuna
kitu cha bure
hakuna
kitu cha bure…”
Kama yule aliyekuwa hasikii basi akiimbiwa
kama ifuatavyo:-
“ Mwari wenu si mwari wee…. Mwari
kinjenje ure..
Mwari wenu si mwari wee…. Mwari
kinjenje ure..”
--Biyaya
(Zanzibar 2015)
Wimbo huu huimbiwa kwa yule
aliyekuwa hasikii (akitumwa hataki hana
heshima) ili asikie basi wazazi wanatanabahishwa wawe imara katika malezi ili
kuzitunza mila na desturi za Zanzibar. Na hii inathibitisha kwamba Zanzibar
mara nyingi watoto wa kike au wakiume hupewa mafunzo mmoja mmoja bila ya
kukusanywa kwa pamoja kama iliyo kwa makabila mengine ya Tanzania bara. Ushahidi
wa hayo Bw. Kayombo F (2014) katika blogsport yake ya kijamii
anatuonesha picha zifuatazo:-
Vijana
Wakiwa katika Mafunzo ya Ujasiri na Kujihami Katika Jando (kulia) na Wasichana
wakiwa Wamejifunika Mablanketi wakiwa Unyagoni (kushoto)
Kwa upande wa michezo ya watoto
ilishajihisha kuimarisha mila na desturi za kizanzibar kwa kuwaeleza watoto
kutenda matendo mema kama kuswali na mashirikiano katika jamii.
Biyaya anabainisha hili kwa kusema:-
“ Miye nikumbukavo twekuwa
tukicheza michezo mingi mfano kama Ntaka Sali. Na twekuwa tukiimba kama hivi:-
“ Ntakaswali wee…salaa ya umande
swalaaa…
Nsimamie wee… salaa ya umande salaa…
Niinamiee wee… salaa. ya umande
salaa…
Niinukie wee.. salaa. ya umande
salaa….”
--Biyaya (Zanzibar 2015)
Kutokana na maudhui ya nyimbo hiyo
ilifunza watoto ingawa walikuwa wakicheza tu mila na desturi zao ziliwataka
waswali swala zote. Na namna ya kuswali ni hivyo kusimama, kurukuu, kusujudu na
vitendo vyengine vinavyofanyika katika kuswali.
4.1
Kufifia au kufa kwa Jando, Unyago na Michezo ya watoto Zanzibar.
Inaaminika kwamba Jando, Unyago na Michezo ya watoto
imefifia au kufa kiutendaji kwa mujibu wa mambo mbali mbali. Mambo haya
yaliendelea kufifia kutokana na kuja kwa wakoloni. Ukoloni ulipokuja umeleta
mabadiliko mbali mbali katika jamii za kiafrika na Tanzania ikiwemo Zanzibar.
Mabadiliko hayo yalikuwa katika Nyanja mbali mbali kama vile elimu, dini, mazingira na sayansi na
teknolojia au utandawazi. Haya
yanathibitishwa na Kayombo, F (2014) katika blogsport yake ya kijamii pale
alipoandika:-
“Malezi ya vijana katika karne hii ya
utandawazi in changamoto nyingi. Vijana wanakosa elimu juu ya ukuaji na
mabadiliko ya mwili waoili waweze kujitambua na kuchukua hatua stahili katika
maisha. Pia wanakosa elimu na ustadi wa kukabiliana na maisha kama wazai,kama
wake au waume. Vitu ambavyo vilikuwa vikifanyika katika unyago na jando lakini
sasa hivi hili halifanyiki kutokana na mila hizi kuachwa kwasababu ya
mabadiliko ya mitindo yetu ya maisha inayoletwa na utandawazi. Utandawazi
unatafsiriwa kuwa ni mfumo wa uhisiano wa kimataifa katika nyanja
mbalimbali kama vile biashara, uchumi au siasa uliowezeshwa na maendeleo ya
teknolojia ya habari yanayofanya mataifa kuwasiliana kiurahisi.”
Tukiichunguza ibara hapo hio inathibitisha
kwamba sanaa za Jando, Unyago na hata Michezo ya watoto kwa kiasi fulani zimepata athari kubwa kwa kukumbwa na wimbi
la utandawazi kama tulivyoona hapo juu. Kwa muktadha huo basi hata Zanzibar
ikiwa ni miongoni mwa sehemu ya dunia haiwezi kukwepa wimbi hilo. Hivyo hivi
sasa ufanyikaji wa sanaa hizi Zanzibar umebadilika tafauti na nyakati zilizopita.
Bi Rahma Abass anasema:-
“ Mimi bahati mbaya
sikuchezwa kama walivyokuwa wakichezwa watoto wa jirani yangu tulipokuwa
tukiishi Sogea, kwa sababu baba yangu yaani nyinyi babu yetu alikuwa ni mtu wa
dini (Shehe). Ila niliwahi kuona mambo kama hayo wakati nipo mdogo sehemu
ambayo ikiitwa Makaburimsafa.
Ilikuwa pana msitu wakati huo. kaka yangu alinipakia kwenye baskeli na
akanambia twende kulee.. wakati huo tulisikia ngoma ikirindima tunakoelekea.
Kwa mbali tulionekana na bibi mmoja aliyetoka katika uwa wa makuti akilalama
kwa mayote kama “ wakamateni hao wakamateni hao si wanataka kuja huku..” kusikia
hivyo tukazitimua mbio na baskeli yetu.”
- Bi Rahma Abass (Zanzibar,
2015)
Bila ya shaka maneno hayo yanatuhakikishia
kwamba sehemu zilizokuwa zikitendwa Jando na Unyago zilikuwa ni maalumu mbali
na makaazi ya watu. Na kwa muktadha huo sehemu hizo kwa wakati tulionao sasa
zimebadilika kama tunavyoona badala ya Makaburimsafa sasa panaitwa Kibandamaiti
na karibuni tu kumebadilika na kuitwa “Uwanja wa demokrasi” sio rahisi tena
kufanywa jando na unyago kama uliyokuwa ukitendwa mwanzo kwa kuwa sasa ni
viwanja na majumba ya watu wakiishi ndani yake, sio msitu tena.
Kadhalika utendwaji wa Jando na Unyago
umebadili muelekeo katika nyakati hizi hapa Zanzibar. Kwa miaka ya sasa sio
rahisi kusikia kuwa watoto wa kike au wa kiume wamewekwa mahali maalumu kwa
kikundi wakifanyiwa Jando na Unyago badala yake wazazi wengi wa Kizanzibari
wanapobaini watoto wao wamebaleghe huwapaleka kwa masomo wao ili kufundishwa
yanayowakabili katika kipindi hicho cha mabadiliko. Na kwa upande wa watoto wa
kiume hufunzwa hayo mara baada ya kutaka kuoa au hujifunza wenyewe kupitia
mitandao ya kijamii ikiwemo FaceBook
, Twitter na WhatApp. Maneno haya yanatiliwa mkazo kwa
maswali mazito na Bw. Kayombo, F (2014) katika blogspot yake akisema:-
“ Hapo awali vijana walikuwa
wakifundwa katika unyago na jando na makungwi walikuwa wakufunzi juu ya mambo
haya na walikuwa na jukumu la kufanya haya kwa niaba ya wazazi na jamii husika.
Lakini sasa hivi kungwi wa watoto wetu ni nani? Mitandao ya kijamii kama
FaceBook ,twitter na WhatApp? TV na Video wanazoangalia usiku na mchana pengine
hata bila mipaka? Je teknolojia hizi zinatoa mafunzo yanayotakikana katika
jamii zetu? Haya yote ni maswali ambayo yanahitaji majibu na hatua za haraka.”
Michezo ya watoto nayo imekubwa na wimbi la
maendeleo ya sayansi na teknolojia. Watoto badala ya kucheza pamoja uwanjani
wakitazamwa na wazazi wao vipenuni mwa nyumba zao, sasa hukimbilia katika
televisheni kwa kuangalia katuni mbali mbali katika sehemu za mashamba ni
mijini. Wakati wa usiku pia watoto hao hukimbilia katika masomo ya ziada
(Tuishen) au madrasa za usiku hasa katika maeneo ya mijini. Mambo hayo huwa yanawakosesha
muda watoto kucheza michezo yao kama ilivyokuwa ikichezwa na watoto zamani.
Kadhalika dini ni moja kati ya sababu
zinazosababisha jando na unyago kufa Zanzibar. Katika jamii za kizanzibar kuna
migongano mbali mbali inayohusu mila na dini. Jando na unyago ni mila za watu
Zanzibar watu hao wakiwa na dini mbali mbali ikiwemo uislamu. Kwa namna moja
ama nyengine unyago unaaminika kwamba ni mila potofu isiyofaa kuendelezwa kwa
misingi ya kiislamu. Haya yanathibitishwa na Irene Brunotti katika Swahili
Forum 12 (2005) katika mada yake isemayo “Ngoma ni uhuni? Ngoma za kisasa mjini
Zanzibar.” Alibainisha kwa kuandika
“Unyago hushirikisha wanaume na wanawake
kama tushuhudiavyo leo. Katika uislamu ni kosa kubwa kwa mwanamme kuchanganika
na mwanamke. Katika unyago huibwa nyimbo za matusi hili halikubaliki hata
kiakili na kimaadili seuze sheria… kwa ujumla huzalikana na kupatikana katika
mila hii ya unyago mambo mengi ambayo yanaghafiriana na sharia … Jamani tuache
mila, desturi na ada hizo potofu na badalaya yake tushikamane na kuzifuata mila
na desturi sahihi za uislamu.”
Katika maandishi hayo tunaweza kugundua
kwamba uislamu ni moja kati ya sababu zinazochangia kufa kwa jando na unyago
Zanzibar kwa kuwa wanajamii wengi wa kizanzibar ni wailamu bila ya shaka mila
na desturi zizoendana na uislamu hulazimika kuzipiga kumbo au kuzikataa.
5.1 Hitimisho
kwa vile Sanaa
hizi (jando, unyago na michezo ya watoto) ni miongoni mwa Sanaa za maonyesho
katika fasihi simulizi zilikuwepo zamani na kutendwa kwa hamasa kubwa na
wanajamii wa Zanzibar. Bila ya shaka zilitoa mchango mkubwa kwa jamii hususan
kwa watoto na vijana kama tulivyoona
hapo juu. Na sasa zinaonekana kufifia au kutoweka utendaji wake ama kufa kabisa
katika jamii. Hivyo iko haja ya kuziendeleza na kuzitunza kiutendaji na
kimaandishi ili ziweze kufaidisha jamii kizazi hadi kizazi.
Kwa kuwa hakuna
jambo lisilo kasoro ulimwenguni bila ya shaka sanaa za jando na unyago haziwezi
kukosa hilo kama vile:-
Kutoa mafundisho kwa watoto ambao
hawajafikia umri unaofaa. Kufungia wasichana au mtoto wa kike (mwari) ndani kwa
muda mrefu mpaka wapate mchumba n.k.
Marekebisho
yanahitajika kwa pale panapohitajika. Mfano katika jando na unyago Mafunzo
juu ya mabadiliko ya kibayolojia wakati wa kubaleghe kwa vijana na hatua za
kuchukua na wakati muafaka wa kuchukua hatua hizo. Mafunzo juu ya kuishi kama
baba au mama kihalali ama mume na mke katika ndoa. Mafunzo juu ya kulinda, kuitunza
na kuijali familia, Uzalendo kwa familia,ukoo,kabila na taifa kwa ujumla ni
mambo ya kuzingatiwa na kuendelezwa katika Sanaa hizi za jando na unyago.
MAREJEO
BAKIZA. (2010). Kamusi la Kiswahili
Fasaha. Kenya. Oxford University Press.
Haji,
A I na wenzake. (1981). Misingi ya
Nadharia ya Fasihi: Taasisi ya Kiswahili na Lugha za
Kigeni/Wizara ya Elimu Zanzibar. Sweden by Berlings, Arlov.
Haji, M. O. (2010). Vipera vya Fasihi Simulizi Tanzania. Kidato
cha 1-4: Kiponda Street Zanzibar.
Medu Press.
John,
J & Mduda, F. (2011). Kiswahili
Kidato cha Tano na Sita. Dar-es Salaam: Oxford University
Press
Kayombo, F (2014). Jando na Unyago:Nini Mbadala Katika Karne
Hii ya Utandawazi?. Iliyoonekana kutoka
http://bongoposts.com/jando-na-unyago-nini-mbadala-katika-karne-hii-ya-utandawazi/
tarehe 20/4/2015.
M,
Mulokozi. M .(1996). Fasihi ya Kiswahili.
Dar es Salaam Tanzania: Chuo Kikuu Huria cha
Mbunda, F.
L .(1996). Mbinu za Kufundishia Lugha ya
Kiswahili. Dar es Salaam, Tanzania: Chuo Kikuu Huria Cha
Tanzania.
Ndumbaro,
E (2013) Sanaa za Maonesho Kabla ya Ukoloni Afrika Mashariki na Mbinu
Zilizotumika Kufifisha au Kuua Sanaa za Maonyesho hapa Nchini. Iliyoonekana
kutoka http://chomboz.blogspot.com/2013/11/sanaa-za-maonesho.html . Tarehe
20/3/2015.
Semzaba,
E .(1997). Tamthilia ya Kiswahili.
Dar es Salaam, Tanzania: Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania.
TUKI.
(2004). Kamusi la Kiswahili Sanifu. Kenya.
Oxford Univerisity Press.