Monday, July 25, 2016

SHAIRI -WINGU

WINGU
  1. Wingu bado limetanda, totoro metugubika,
            Kimbunga kinajiwinda, si dhani kama tavuka,
              Kiza nacho kimewanda, au ndo hayo masika?
              Wingu bado limetanda, mvua ndoto kunyeka.

  1. Kiza bado kimewanda, mvua imetoweka,
            Mipunga bado mikinda, vigumu kunawirika,
            Ndege nayo waiwinda, wataka kunufaika,
            Wingu bado limetanda, mvua ndoto kunyeka.

  1. Mipango nayo ni shinda, kumwagilia mashamba,
             Imekuwa ndugu donda, vipi litatuponyeka,
             Donda hili limevunda, harufu yake yanuka,
             Wingu bado limetanda, mvua ndoto kunyeka.

  1. Aridhi nayo ndandanda, kwa jembe ngumu limika,
            Wakulima yatushinda,  kuiburuga hakika,
            Mihindi tuloipanda, pole pole yanyauka,
            Wingu bado limetanda, mvua ndoto kunyeka.

  1. Wamechoka nao punda, nasi pia twahenyeka,
             Maji yamekuwa shinda, na ni machafu kunyweka,
             Wingu hili latutenda, lini tutaneemeka,

             Wingu bado limetanda, mvua ndoto kunyeka.

Tuesday, February 2, 2016

HATUA ZA KUFASIRI MATINI.


HATUA ZA KUFASIRI MATINI ZA AINA MBALI MBALI.
Mwansoko na wenzake (2006) Tafsiri ni zoezi la uhawilishaji (Transferring) wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.

Merinyo, F. A (2014) akimnukuu Mshindo (2010:2) anasema kufasiri ni kufafanua maana ya matini moja na kutayarisha baadae matini nyengine inayowiyana nayo ambayo huitwa tafsiri na ambayo inawakilisha ujumbe ule ule uliomo katika matini ya awali kwa kutumia lugha nyengine.

Wataalamu mbali mbali wameainisha hatua kadhaa za kufuatwa katika mwenendo mzima wa kufasiri matini mbali mbali. Katika kujadili swali hili tutajadili hatua saba (7) kama zilivyoainshwa na Mwansoko na wenziwe  (2006). Hatua hizo ni kama ifuatavyo:

Hatua ya maandalizi, uchambuzi, uhawilishaji, rasimu ya kwanza, udurusu wa rasimu ya kwanza, kusomwa kwa rasimu na mtu mwengine na usawidi wa rasimu mwisho.


Hatua ya kwanza ni hatua ya maandalizi. Hatua hii inahusisha mambo matatu ambayo ni  Kupitia sehemu muhimu za matini chanzi, kwa mfano; istilahi, majina ya wahusika, majina ya kijiografia, maeneo au kauli zisizofasirika kirahisi. Kupata marejeleo ili kutafuta visawe vya kisemantiki. Kutafuta na kuandika visawe hivyo. Kadhalika hatua hii mfasiri huchunguza taarifa zinazohusu usuli wa matini chanzi. Hizi ni taarifa zinazohusu mwandishi wa matini, mazingira ya uandishi wa matini chanzi, malengo yake, utamaduni wa wazungumzaji wa matini chanzi na hadhira lengwa ya matini chanzi. Katika kuudurusu usuli wa matini chanzi mfasiri pia anapaswa kuzingatia sifa za kiisimu za matini anayotaka kuifasiri. Wakati huo huo mfasiri huandika pembeni (kwenye daftari maalumu) misamiati na istilahi muhimu maneno ya kitamaduni na sehemu ngumu katika matini chanzi ambazo zinahitaji uchunguzi na utafiti zaidi. 

Hatua ya pili ni uchambuzi. Katika hatua hii mfasiri huchunguza kwa makini maneno pamoja na maelezo muhimu ya matini chanzi aliyoyaandaa katika maandalizi ili aweze kuyatafutia visawe stahili katika lugha lengwa. Zoezi la uchambuzi hufanywa kwa kutumia marejeo mbali mbali, kama vile kamusi. Inashauriwa kuwa mfasiri awe na buku na notisi au faili kwa ajili ya kuandika na kuhifadhi maneno na maelezo muhimu na visawe vya matini chanzi. Visawe vilivyokubalika viorodheshwe vizuri ili iwe rahisi kurejelewa wakati wa kufasiri. Ikiwa matini chanzi ni kubwa sana mfasiri huwa hana budi ila ni kuigawa katika sehemu ndogo ndogo kama sura, aya na sentensi na kuitafasiri sehemu moja baada ya nyengine. Hata hivyo inashauriwa kwa mfasiri kwamba aya iwe ndio kizio cha msingi katika tendo la kufasiri.     


Hatua ya tatu baada ya maandalizi ni uhawilishaji (transferring/transference). Katika hatua hii mfasiri huhawilisha ile taarifa kutoka kwenye matini chanzi kwenda kwenye matini lengwa, hapa mfasiri anatakiwa kuzingatia sarufi ya lugha lengwa na lugha chanzi. mfano; “My new house is broken”-Yangu jipya nyumba ni vunjika. Tafsiri ya Kiswahili fasaha inapaswa kuwa “Nyumba yangu mpya imebomoka” Uhawilishaji maana yake ni kuhamisha maana, ujumbe nk. kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa kwa kuzingatia sarufi ya lugha lengwa, lengo la matini au mwandishi, umbo la matini, mtindo nk.
Mbinu ya tafsiri ambayo inatumika katika hatua hii ya uhawilishaji ni tafsiri ya neno kwa neno.


Kadhalika hatua ya nne ni kusawidi rasimu ya kwanza (drafting). Uhawilishaji wa visawe kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa unapokamilika kinachopatikana ni rasimu ya kwanza ya tafsiri. Rasimu ni kitendo cha kuandika matini au Makala yoyote kwa mara ya kwanza kwa mujibu wa utaratibu BAKIZA (2010). Mfasiri anapoanza kusawidi rasimu ya kwanza ya tafsiri yake atashuhudia kuwa anahitaji taarifa au ufafanuzi zaidi kuhusu uchambuzi aliokwishafanya mwanzo. Kwa hivyo atalazimika kufanya uchunguzi zaidi usuli wa matini na hata kupekuwa tena kamusi na marejeo mengine aliyotumia. Pia anapofanya uhawilishaji wa maana, mfasiri inafaa azingatie umbo la matini chanzi kuhakikisha kuwa linaakisiwa na matini lengwa. Mfano iwapo matini chanzi ni shairi la tathlitha (mistari mitatu) sura au umbo hilo halina budi kurudiwa katika matini lengwa. Akiwa nasawidi rasimu ya kwanza mfasiri inafaa afikirie hadhira anayoilenga pamoja na lengo la matini chanzi, kwani mambo haya huathiri mno usawidi wa tafsiri. Rasimu ya kwanza ya tafsiri inakuwa na dosari nyingi na kwa hiyo haifai kupelekwa kwa mteja au hadhira. Badala yake rasimu ya kwanza lazima ipitiwe tena na kurekebishwa au kudurusiwa.


Vile vile hatua ya tano ni kudurusu rasimu ya kwanza ili kuunda rasimu ya pili. Mfasiri hupata fursa ya kwanza ya kuitathimini na kuifanyia marekebisho tafsiri yake mwenyewe. Kazi ya kudurusu haipaswi kufanywa haraka. Wataalam wengine kama vile Larson (1984) anasema rasimu ya kwanza ni lazima iachwe kwa muda wa wiki moja. Udurusu unahusisha shughuli zifuatazo:
Kusahihisha makosa ya kisarufi, miundo isiyoeleweka vizuri.

Kunyoosha sehemu zenye tafsiri ya mzunguko na zenye matumizi potofu ya visawe. Mfano; “They rarely visit me these days – Siku hizi ni aghalabu-nadra sana wao kunitembelea.” Kurekebisha sehemu zenye muunganiko tenge au mbaya ambazo zinazuia mtiririko mzuri wa matini. Kuhakiki usahihi na kukubalika kwa maana zinazowasilishwa katika matini lengwa. Hapa tunaangalia kama kuna mambo yameongezwa, yamepunguzwa au yamepotoshwa/kubadilishwa. Kuhakiki kukubalika kwa lugha uliyotumia katika tafsiri yako kwa kuzingatia umbo na mada ya matini chanzi.
Kuona iwapo mada au ujumbe mkuu wa matini chanzi unajitokeza waziwazi katika matini lengwa.

Baada ya kuzingatia masahihisho hayo mfasiri atalazimika kutoa rasimu yake ya pili ambayo inashauriwa ampe msomaji mwengine ili aidurusu na kupendekeza masahihisho zaidi. Jambo hili litasababisha kwenda hatua nyengine inayofuata katika mwenendo wa kufasiri.

Kwa kuendelea hatua ya sita  ni kusomwa rasimu ya pili na mtu mwingine. Msomaji wa rasimu ya pili anaweza kuwa mfasiri au shabiki wa tafsiri, mhakiki au mhariri wa tafsiri, anaweza kuwa mpenzi wa tafsiri mbali mbali au mtu mwingine yeyote anayemwamini mfasiri. Katika hatua hii mfasiri anashauriwa atumie mbinu zifuatazo katika kumpata mtu mwengine ili kuisoma tena rasimu ya pili Kumpa bila kumjulisha kwamba ni tafsiri kumpa matini chanzi na matini lengwa ili alinganishe. Inapendekezwa kwamba mtu huyo asome kwa sauti ili uweze kubaini upungufu na iwapo atafikia pahala na kusita katika usomaji wake basi uwezekano mkubwa wa sehemu hizo za matini kuwa zina matatizo ya kiufasiri matatizo hayo yanaweza kuwa ni matumizi potofu ya viunganishi vya sentensi, upotoshaji wa maana za maneno, uendelezaji mbaya wa maumbo ya maneno au mikanganyiko katika matumizi ya mitindo. Hali hii ikitokea mtu aliyepewa kuidurusu rasimu ya pili atalazimika kuweka alama maalumu sehemu zenye matatizo na kisha kumuelekeza mfasiri azichunguze tena na kuzirekebisha.


Na mwisho ni hatua ya saba nayo ni kusawidi rasimu ya mwisho. Katika hatua hii mfasiri atafanyiakazi maoni na mapendekezo ya msomaji ambaye alimpa kazi yake. Matokeo ya kufanyiakazi maoni husababisha kupatikana kwa rasimu ya mwisho ambayo ndiyo humfikia mteja, hadhira, wachapaji na wengineo wanaolengwa iwafikie.

Hizi ndizo hatua zinazofaa kufuatwa katika mwenendo wa kufasiri matini za aina mbali mbali. Hata hivyo katika mwenendo halisi wa kufasiri inawezekana hatua hizi zisifuatwe katika mpangilio ulielezwa hapo juu. Hii ni kwa kuwa na ukweli kwamba wakati wa tendo la kufasiri mfasiri hulazimika daima kwenda mbele na nyuma kutoka katika matini chanzi mpaka kwenye matini lengwa. Pamoja na hayo ni muhimu kwa mfasiri kutambua kuwa kuna hatua zilizotajwa hapo juu katika mwenendo mzima wa kufasiri matini mbali mbali ambazo ni vyema kuzifuata kila inapowezekana.
 

MAREJEO.

Merinyo, F. A (2014). Tafsiri na Ukalimani (Utangulizi Muhimu katika Tafsiri

                               na Ukalimani). Mkuu-Rombo. Tanzania.

Cartford, J. C. (1965). A Linguistic Theory of Translation. London: OUP.
Larson, L. M. (1984). Meaning-based Translation. London: University Press

                               of America.
Mwansoko, H. J. M. na wenzake (2006). Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na

                                                         Mbinu. Dar es Salaam: TUKI

BAKIZA (2010). Kamusi la Kiswahili Fasaha. OUP. Nairobi Kenya.
 

Tuesday, January 19, 2016

FASIHI NA UISLAMU


YALIYOMO

                  1.0       Utangulizi.

1.1              Miongoni mwa tabia na mwenendo mwema unaosabisha mja kuipata shahada mwisho wa maisha yake. 

1.2              Matendo mabaya na maovu yanayosababisha mja kukosa shahada wakati

wa kifo chake.

2.0      Hitimisho.  

1.0              Utangulizi

Uislamu ni mfumo kamili wa maisha na ndio dini inayokubalika na muumba wetu kama alivyosema katika Qur-ani kwamba dini anayoikubali M/Mungu ni uislmau. Kupitia hadithi ya Mtume iliyotoka kwa Abdur-Rahman Abdullah bin Umar bin Khattwab (r.a) anasema: Nimemsikia Mjumbe wa Allah (S.A.W) akisema “Uislamu umejengwa juu ya mambo matano: kushudia ya kuwa hakuna mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah na kuwa Muhammad ni Mjumbe wa Allah na kusimamisha swala na kutoa Zaka na kuhiji Nyumba Tukufu, na Saumu ya Ramadhan.” (Bukhar na Muslim). Tukiichunguza hadithi hii kwa makini inatuhakikishia kwamba “Kushudia ya kuwa hakuna mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila ni Allah na kuwa Muhammad ni Mjumbe wa Allah. Ndio nguzo ya kwanza inayousimamisha uislamu na mja hana budi ili afanikiwe hapa duniani na akhera ni budi aishi kulingana na maamrisho aliyoyaamrisha Allah na Mtume wake, na ayaepuke yale yote yaliyokatazwa na Allah na Mjumbe wake.

Kwa mkabala wa kiislamu hakika hakuna tafauti ya dunia na dini ila kuna mambo ya kiislamu na yasiyokuwa ya kiislamu. Bila ya shaka jambo ambalo litaundwa kwa misingi ya kiislamu litakuwa la kiislamu kwa hivyo tamthilia ya “Shahada” imejaribu kwa kiasi kikubwa kuonesha matendo mbali mbali ambayo mtu akiyafanya huwa ni sababu mwisho wa maisha yake kuipata shahada na kuwa mja mwema. Kinyume chake imejaribu kuonesha matendo maovu ambayo yatamfanya mtu kujuta mwisho wa maisha yake na kuikosa shahada. Matendo hayo yameoneshwa kupitia wahusika walioicheza tamthilia hiyo kama vile Salami (Mume wa Mama Afrah na mwajiriwa wa Bw. Zuberi), Samira (Mke wa Zuberi), Zuberi (Mwajiri wa Salami), Kifimbo (Rafiki wa Zuberi na Salami) na wengineo ambao wamebeba dhima mbali za tamthilia hii.

 Katika tamthilia ya “Shahada” tunajifunza kwamba tabia njema ndio ufunguo wa kuipata shahada katika maisha ya muislamu. Kama Mtume alivyowahimiza waumini kujipamba na tabia njema.

 Kutoka kwa Abdalla bin Amr (r.a) anaeleza kuwa Mtume wa Allah amesema “Aliyekipenzi changu kuliko wote katika nyinyi (waislamu) ni yule aliyewazidi kwa tabia njema” (Bukhari). Katika Imani ya kiislamu kushuhudia kuwa Mtume Muhammad ni Mjumbe wa M/Mungu na kufuata aliyoyaelekeza kupitia suna yake ndio shahada ya pili.

Pia kutoka kwa Abu Hurairah (r.a) amesimulia kuwa Mtume (S.A.W) aliulizwa juu ya mambo yatayopelekea watu wengi kuingia peponi, akajibu Mtume “Uchaji mungu na tabia njema.” Kisha akaulizwa tena ni mambo yepi yatakayompelekea mtu kuingizwa motoni? Alijibu Mtume (s.a.w) “Mdomo na tupu (viungo vya siri)” (Tilmidhy).

Hivyo muumini wa kweli hana budi kujipamba na vipengele vya tabia njema vilivyoainishwa katika Qur-ani na Sunna ili iwe rahisi kuipata shahada mwisho wa maisha yake hapa ulimwenguni. 

 

1.1 Miongoni mwa tabia na mwenendo mwema unaosabisha mja kuipata shahada mwisho wa maisha yake. 

Kujielimisha kwa ajili ya Allah. Ni katika vipengele vya tabia njema ambayo mja humfanya kuipata shahada mwisho wa maisha yake. Kwa kupitia tamthilia ya “Shahada” Salami mwanzo kabisa wa tamthilia anatuonesha kuwa yeye ameshikamana na maisha ya kheri (kwamba ameshudia ya kuwa hakuna mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah na kuwa Muhammad ni Mjumbe wa Allah) na kupitia maisha hayo yanaashiria mwisho mwema wa maisha yake. Salami anatuonesha kuwa ni mtambuzi wa mambo katika maisha yake. Na bila ya shaka alijielimisha kwa ajili ya Allah. Hapa tunaona Salami alimsitiri muislamu mwenziwe alipopata ajali na kufariki dunia. Alishiriki kikamilifu katika kumuosha na hatimae kumzika. Bila ya elimu matendo haya asingeweza kuyatenda. Elimu ndio zana aliyotunukiwa mwanaadamu ili aitumie kutekeleza majukumu yake hapa ulimwenguni. Kama Qur-ani inavyosema. “Je wanaweza kuwa sawa wale wanaojua na wale wasiojua?” wanaotanabahi ni wale wenye akili tu.” (39:9) Na ni hakika sio sawa baina ya Salami na wale waliokimbia na gari baada ya kumgonga muislamu mwenzao na kusababisha kifo chake bila ya kujali.  

Kuwa na hekima. Hekima ni katika vipengele vya tabia njema vilivyoazizi anavyotakiwa avipiganie muumini ili awe na hadhi inayostahiki na ili aipate shahada mwisho wa maisha yake. Qur-an (2:269) “Allah humpa hekma amtakaye na aliyepewa hekma bila ya shaka amepewa kheri nyingi. Na hawakumbuki ila wenye akili.” Hiki ni kipengele chengine cha tabia njema kama kinavyooneshwa katika tamthilia ya “Shahada”. Na hapa tunaoneshwa kupitia muhusika Samira alipokuwa akimkumbusha Salami maovu yaliyofanywa na mumewe Zuberi kwa kusema “Si unajua alivyo kisirani, si unakumbuka jana alivyokuwa akikufanya. Yani hivi vitendo havipaendezewi  kabisa kibinaadamu. Na Nilivyoumia! Sana.” Salami alionesha wingi wa hekima kwa kutoa maneno ya hekima na msamaha na kutaka aombewe dua ili ajuwe anachokifanya kwani hayo aliyoyafanya kwa kutokujua kwa kusema “ Basi tumsamehe tu kwa sababu yeye hajui atendalo tunachotakiwa kumuombea dua na mungu amsaidie na sio vizuri tena kumuongelea” . 

Kadhalika Ikhalas ni katika vipengele vya tabia njema inayoweza kusababishia mtu kuipata shahada mwisho wa maisha yake. Ikhlasi ni kufanya kila jambo jema kwa ajili ya Allah tu. Yaani kutoa huduma na mali kwa watu wanaohitaji msaada bila ya kutarajia malipo yoyote kutoka kwao ila kutoka kwa Allah (s.w) Kwa Mfano kumlisha na kumvisha fukara, masikini au yatima bila ya kutarajia hata kupata shukurani kutoka kwake ila tu kwa kutegemea malipo kutoka kwa Allah. Qur-an (76:8-10) “Na huwalisha chakula masikini na yatima na wafungwa na hali ya kuwa wenyewe wanakipenda chakula hicho. Husema moyoni mwao wanapowapa chakula hicho tunakulisheni kwa ajili a kutaka radhi ya M/Mungu tu. Hatutaki kwenu malipo wala shukurani. Hakika sisi tunamuogopa mola wetu hiyo siku yenye shida na tabu” Hali hii inajitokeza pale ambapo Bibi kipofu na mwanawe walipokwenda kwa  Tajiri Zuberi kuomba msaada. Zuberi kwa kiburi na jeuri na hata kuwapiga alikataa kuwapa msaada walioutaka. Lakini Salami alionesha wingi wa ikhlas kwa kuwasaidia watu hawa bila ya kutarajia malipo kutoka kwao kwa kuwa alikiri kuwa hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Allah na Mtume (S.W.A) ni mjumbe wake.   

 

Kujiepusha na riya na kujiona. Pia ni kipengele cha tabia njema ambacho humfanya mja kuipata shahada mwisho wa maisha. Riya ni kinyume cha ikhlasi. Kufanya riya ni kufanya jambo jema ili watu wakuone wakusifu wakupe shukurani. Mtu anaefanya riya hafanyi wema kwa kutarajia malipo kutoka kwa Allah (s.w) bali hufanya kwa kutarajia malipo ya hapa duniani tu iwe ni mali, sifa au shukurani. Haya tunayapata pale Salami alipomlipia Kifimbo alipokuwa akidaiwa na kushurutishwa kulilipa deni wanaomdai bila ya kuwa na uwezo wa kulilipa. Salami aliyafanya haya bila ya kutaraji sifa au shukurani ila ni kutaraji malipo kutoka kwa Allah. Qur-ani (11:15-16) M/Mungu anasema “Wanaotaka maisha ya dunia na makombo yake, tutawapa huku duniani (ujira wa) vitendo vyao kamili humu wao hawatapunjwa. Hao ndio ambao hawatakuwa na kitu katika akhera ila moto na wataruka patupu walioyafanya katika dunia hii na yatakuwa bure waliyokuwa wakiyatenda.

 

Kujiepusha na zinaa na tabia za kizinifu. Hiki pia ni kipengele cha tabia njema ambacho bila ya shaka mja akidumu nacho huwa ni sababu kwake kuipata shahada. Waumini wa kweli waliofuzu hujihifadhi na zinaa au kujiepusha kufanya jimai nje ya mipaka iliyowekwa na Allah (s.w). Muumini wa kweli aliyekiri kuwa hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Allah na Mtume ni Mjumbe wake hutekeleza bila ya kusita ile amri ya Allah (s.w) ya katazo la “ Wala usiikaribie zinaa kwa hakika huo ni uchafu na ni njia mbaya kabisa . (17:32). Katazo hili alilitekeleza Salami katika tamthilia ya “Shahada” na nikutokana na hilo ndio ikawa chanzo cha kifo chake na alikufa akiitoa shahada kwamba ameshuhudia kuwa hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Allah na Mtume ni Mjumbe wake. Mbali na vishawishi vya Samira mke wa mwajiri wake kumlazimisha kutembea nae lakini Salami alikuwa na msimamo na kukataa katakata. Matendo haya mema na mwenendo wa muhusika Salami ndio yaliyosababisha Salami kufa kifo chema cha kuitamka shahada. Hivyo ni kweli kwamba kuipata shahada kunategemea na maisha anayoishi mja.   

 

1.2 Matendo mabaya na maovu yanayosababisha mja kukosa shahada wakati wa kifo chake.

Kinyume chake kwa matendo maovu na mwenendo mbaya ni sababu kubwa kwa mja kushindwa kuitamka shahada mwisho wa maisha yake hapa ulimwenguni. Na ushahidi kamili tunaupata mwisho Zuberi alijutia yote aliyoyafanya na kushidwa kuipata shahada wakati wa mauti yake yalipomfikia. Miongoni mwa matendo hayo maovu yaliyomkosesha shahada Zuberi na wenzake kama Kifimbo ni kama yafutayo:-

Dharau. Hiki ni kipengele kimoja wapo cha mwenendo mbaya ambacho huweza kumuepusha mja kuitamka shahada mwisho wa maisha yake. Mwenye kuwadharau wengine hujihisi kuwa yeye bora kuliko mwengine. Hili ni kosa kubwa kwani anayejua aliye mbora ni Allah (s.w) Pekee kama tunavyojifunza katia Qur-an. “Enyi watu! Kwa hakika tumekuumbeni (nyote) kutoka kwa (yule) mwanaume ; Adam na yule mwanamke (mmoja; Hawwa). Na tumekufanye mataifa na makabila (mbali mbali) ili mjuane. Hakika ahishimiwaye sana miongoni mwenu mbele ya M/Mungu ni yule amchaye Mungu Zaidi katika nyinyi…” (49:13). Tajiri Zuberi alimdharau sana Salami, alimuona mjinga sana hata kumwita “Bwege nazi mkubwa”, “Kelbu mkubwa”, “Mshenzi wewe” “Shuwaini”,  Kenge maji”, “Punda”. Haya na mengine ndio yaliyomsababisha Tajiri Zuberi kuikosa shahada wakati wa kifo chake.

Tabia ya matusi na maneno machafu. Pia ni mwenendo mbaya ambao bila ya shaka huweza kumzuia mja wakati wa kutoka roho yake kuitamka shahada. Tajiri Zuberi alikuwa na matusi na maneno machafu katika kinywa chake kwa lengo la kumdhalilisha Salami. Kwa waislamu kuna katazo kubwa juu ya hilo. Tumekatazwa kutukanana na hata kuitana majina tusiyoyapenda kwa kejeli. M/mungu katika Qur-an anasema “…Wala msitukanane kwa kabila wala msiitane majina mabaya (ya kejeli). Jina baya kabisa kuitwa mtu ni “Fasiq” baada ya kuwa yeye ni muislamu. Na wasio tubu basi hao ndio madhalimu. (49:11). Tukirejea mafundisho ya Mtume tunayapata kupitia hadithi kutoka kwa Abu Hurairah (r.a) amesimulia kuwa Mtume (S.A.W) aliulizwa juu ya mambo yatayopelekea watu wengi kuingia peponi, akajibu Mtume “Uchaji mungu na tabia njema.” Kisha akaulizwa tena ni mambo yepi yatakayompelekea mtu kuingizwa motoni? Alijibu Mtume “Mdomo na tupu (viungo vya siri)” (Tilmidhy). Kwa hiyo jambo moja kubwa alilokuwa nalo Tajiri Zuberi ni Mdomo mchafu na huu ndio uliomkosesha kuitamka shahada wakati wa kifo chake.

Kadhalika kutokuwa na huruma. Ni miongoni mwa mwenendo mbaya ambao humzuia mja kuikosa shahada mwisho wa maisha yake. Tajiri Zuberi alijipamba na mwenendo huu ovu wa kutokuwa na huruma. Aliwashambulia masikini waliokuwa na mahitaji kwa jeuri na kiburi na mwisho kuwafukuza bila ya huruma kwake na haya ndio yalikuwa maneno yake walipokuwa wakijibizana na masikini waliokuja kutaka msaada. “ Kwanza nani aliyewatuma mje hapa? Hivi mimi naweza kuzaa mjusi kama wewe! Nakuuliza naweza kuzaa mjusi kama wewe? Na wewe mama kipofu umepita majumba yote huko hukuona pakuingia isipokuwa huku eh! Nikusaidie nini? Toka hebu kwenda huko na wee mama nenda huko pumbavu! Kwendeni!”

Muunini wa kweli hana budi kujipamba na tabia ya kuhurumia viumbe  wenzake. Amuonee huruma kila mwenye shida na ajitahidi kumsaidia inavyowezekana. Katika kuonesha umuhimu wa kipengele hiki katika uislamu Mtume (s.a.w) amesema “Ambaye hahurumii watu, pia Allah (s.w) hatamhurumia” (Bukhari). Huruma hudhihiri katika kuwasaidia wenye shida na matatizo kwa mali na kauli kama Qur-ani inavyotufunza “ Hamtaweza kufikia wema mpaka mtoe katika vitu mnavyovipenda na chochote mnachokitoa, basi hakika Allah anakijua”. (3:92). Tabia hii mbaya ya kutokuwa na huruma kwa wenye shida ndio moja miongoni mwa nyingi zilizomponza Tajiri Zuberi kuikosa shahada wakati wa kifo chake.

 

Unafiki ni miongoni mwa tabia mbaya na ovu kwa muumini. Mnafiki ni yule anaekubali uislamu mdomoni (kwa kauli tu) lakini moyoni mwake na katika matendo yake anaukanusha. Kupitia Qur-an (2:8-9). “ Na katika watu wako wasemao tumemuamini M/Mungu na siku ya mwisho hali ya kuwa wao si wenye kuamini. Wanataka kumdanganya Allah na wale walioamini, lakini hawadanganyi ila nafsi zao, nao hawatambui”. Kifimbo kaonesha unafiki pale anapokuja kwa Salami muislamu mwenziwe ni mtu mwema wakati huo huo akenda kazini kwake anamchongea kwa mwajiri  wake. Na akirudi tena kwa Salami humchonganisha yeye na mkewe, na hatima yake mke wa Salami kuomba talaka kwa mumewe kwa unafiki wa Kifimbo kusema kuwa Salami ana mke mwengine. Matendo haya ya Kifimbo ni ya kinafiki na ni matendo maovu ambayo yanaweza kuwa sababu kwa mja kuikosa shahada mwisho wa maisha yake.

Kiburi na majivuno. Kiburi, majivuno na majigambo ni katika tabia mbaya iliyokemewa vikali katika Qur-an kama ifuatavyo (31:18). “Wala usiwatazame (watu) kwa upande mmoja wa uso, wala usiende katika ardhi kwa maringo, hakika Allah hampendi kila ajivunae ajifaharishaye” Zuberi anajiona kuwa ni bora kwa Salami na ni wajuu na wa maana zaidi kuliko Salami. Kiburi hicho na kujiona kulisababishwa na neema (utajiri) aliotunukiwa na mola wake. Tabia hii ovu ndio iliyokuwa sababu kwa tajiri Zuberi kujuta na kuikosa shahada wakati kifo kilipomfikia.

Kuikimbilia zinaa na tabia za kizinifu. Ni miongoni mwa tabia mbaya ambayo ni moja kati ya zile zinazoweza kumzuia mja kuipata shahada mwisho wa maisha yake. Katika tamthilia ya “Shahada” tumeoneshwa Samira (mke wa tajiri Zuberi) ni mwenye kuikimbilia zinaa na ni mwenye tabia za kizinifu. Samira alifanya kila analoweza kumrubuni Salami atekeleze matamanio yake anayotaka. Alimpa pesa sio kwa kumsaidia bali kwa lengo la kumhonga. Hatima yake alimfungia milango kwa kumlazimisha afanye nae zinaa japo kwa mara moja tu. Na jambo hili ndio sababu kwa mumewe kumteka Salami na kumuadhibu. Na pia ndio sababu kupoteza maisha yake bila ya kuipata shahada. Mwenendo huu na tabia hii ya uzinifu sio tabia njema kwa muumini aliyeshuhudia  kuwa hakuna mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah na kuwa Muhammad ni Mjumbe wa Allah.  


2.0 Hitimisho

Kupitia tamthilia ya “Shahada” ni dhahiri kwamba kuipata shahada mwisho wa maisha ya mja duniani kunategemea na jinsi anavyoendesha mja maisha yake. Haya yanathibitika kupitia muhusika Salami ambapo maisha yake yote aliishi kwa kujipamba na tabia njema na kutennda yaliyo mema kama vile kujielimisha kwa ajili ya Allah kwa kutenda matendo mema kwa ujuzi na elimu sahihi, kuwa na hekima, kuwa na ikhlasi, kujiepusha n aria, na kujikinga na zinaa. Na kinyume chake kuikosa shahada kunategemea na mwenendo wake hapa ulimwenguni. Haya tunaoneshwa na Tajiri Zuberi katika tamthilia ya “Shahada” pale alipojipamba na tabia mbaya na mwenendo mbaya kama vile; kuwa nadharau, kuwa na tabia ya matusi na maneno machafu, kutokuwa na huruma, na kuwa na kiburi na majivuno ya kupindukia. Haya na mengineyo ndio sababu kwake kuikosa shahada mwisho wa maisha yake.   


MAREJEO

Al-farsy, A. S (1993).Qur-an Takatifu, The Islamic Foundation. Nairobi Kenya.

An-Nawawi, Y. S (2009). Matnu Arbain Nawiyyah na Tafsiri yake. Ibn Hazm Media Center. Dar-es-salaam. Tanzania.


IPC. (2003). Nguzo za Uislamu, Darasa la Watu Wazima Juzuu ya 2. Islamic Propagation Centre DSM. Tanzania.

 

 

 

 

Monday, December 21, 2015

SWALA NI AMALI ADHIMA


Swala  amali adhima.

 

1.     Swala tano ni lazima,         kwa mumini isilama,

          Lazima afanye hima,          kuziswali kiheshima,

          Nathawabu atachuma,        kwa mzima na kilema,

          Isilamu hima hima,            swala amali adhima.

2.     Dada haya jisukuma,         Jumamosi na Ijuma,

Adhana ikilalama,              itika nawe kusoma,

Kaswali usiwe nyuma,       ukazivune neema

          Isilamu hima hima,            swala amali adhima.

3.     Kwenye siku hurindima,   tano huwa kusimama,

Adhuhuri nikisema,            ni rakaa nne nzima,

Tekeleza isilama,              swala ni nguzo nzima

          Isilamu hima hima,           swala amali adhima.

4.     Laasiri si hekima,             kuiacha ikikoma,

Magharibi kwa heshima,  kaswali ni jambo jema,

Tenda ukiwa mzima,        Pandu na wewe Salama,

          Isilamu hima hima,           swala amali adhima.

5.      Isha, fajir simama,           uondoshe yako dhima,

Safisha yako khatima,      uwe salama kiyama

Uiepuke nakama,              kwenye moto jahanama,

          Isilamu hima hima,           swala amali adhima
 

 

 

 

 
 
    

Monday, November 30, 2015

ELIMIKA KWA SHAIRI


3         KILA KIINGIACHO MJINI…

1.      Hivi kweli kila kiingiacho, mjini ni halali?

      Insi wakubali kila kinenwacho, ughaibuni ni halali!

      Maana waungama nacho, wakionapo runingani.

 

2.      Twakubali kwani tunamacho, hata hatuoni mbali!

      Ya ukweli na yasokificho, twabaini kila hali,

       Hii ni kweli kila kiingiacho, mjini ni halali?

 

3.      Kina dada wafanyacho, miilini wameridhi na kukubali!

      Wakwatuwa rangi zao na kubadili macho, ja shetani au si kweli?

      Watutumuwa maungo yao bila kificho, nasi twakubali

       Hii ni kweli kila kiingiacho, mjini ni halali?

 

4.      Kina kaka wakata mikato, ya kila sampuli

      Wafuasi kwa kila wakisikiacho, kwao ni makubuli

       Na wanafakhari watendacho, hata kama sicho kwa staili

       Au ndio kweli kila kiingiaho, mjini ni halali!

 

5.      Waduchu wafungua macho, wayaona nayo wayanakili,

      Wayadizaini, wayafuma na kuyaunda, mwisho, huwa makali kama pilipili,

      Waling’amua hawa kwa wakuu  wakifanyacho, alimradi kisulisuli!

      Ama kweli! Kila kiingiacho, mjini ni halali!

 

 

 

6.      Methali ni zetu kweli twazikubali!

      Kama fuata nyuki ili ule asali,

      Au chovyachovya hatimae, humaliza buyu la asali,

      Ama kilio huanza mfiwa, ndipo wa mbali,

      Na ile ya kivuli cha mvumo, hufunika aliye mbali,

       Pia ya mchele je! Mmoja, mapishi  ni mbali mbali,

       Ila nyengine si stahili, maana za umiza matumbo kweli,

        Kila kiingiacho mjini ni halali? Hii yanipa mushikeli.

 

SOMA SHAIRI UNUFAIKE


1.      TATA

1.      Ta! ta! Naanza kwa tata, kunena yanotokota,

      Tata hili lasokota, vichanga linaambata

      Wakuu nao wajuta, kwanini lawafuata

       Tata hili tata gani? Bado linatukung’uta.

 

2.      Juhudi zinatusuta, kulitokomeza tata,

      Kila leo tunateta, Bado limetufumbata,

      Twapiga ngumi ukuta, aah! Twajikunyata,

      Tata hili tata gani?  Bado linatukung’uta!  

 

3.      Sasa mwishoni nasita, na tena najiokota.

      Ta! Hili si la kugatwa, nanena tena nateta,

      Ogopa sije kudota! Utakuja kuufyata,

 

                        Tata hili tata gani?  Bado linatukung’uta.

 

Monday, April 27, 2015

KUIMARIKA NA KUTOWEKA KWA JANDO UNYAGO NA MICHEZO YA WATOTO ZANZIBAR



Kukua au kuimarika na kufifia au kufa kwa Sanaa za maonyesho.
(Jando, Unyago na Michezo ya watoto)
1.      Utangulizi
Sanaa za maonyesho zimekusanya vipengele mbali mbali, vipengele hivyo ni kama:- Sherehe mbali mbali (harusi, siasa), ngoma mabali mbali,  masimulizi ya hadithi,  kusalia miungu,  majigambo,  ngonjera, tamthilia, michezo ya watoto, jando, unyago, utani na nyenginezo. Vipengele hivyo kila kimoja kinamaana inayojipambanua na kipengelele chengine katika utendaji wake. Kadhalika sanaa za maonyesho namna zilivyokuwa zikitekelezwa zamani ni tafauti na zinavyotendwa sasa. Hali hii ya utendaji hubadilika kulingana na nyakati, husababishwa na mambo mbali kama vile maendeleo ya sayansi na teknolojia, dini, mitazomo ya watendaji (fanani na hadhira) na hata hali ya mabadiliko ya mazingira katika jamii zinazohusika. Sanaa za maonyesho au tendaji hutendwa kwa namna mbali mbali kulingana na jamii inayohusika.  Tanzania ikiwemo Zanzibar sanaa hizi za maonyesho hutendwa au hutekelezwa kwa namna tafauti na jamii nyengine nje ya Tanzania.  Katika Makala haya tutajadili na kufafanua namna Sanaa za maonyesho (Jando, Unyago na Michezo ya watoto) zilivyoshamiri hapo mwanzo na namna zinavyofifia au kufa kwa sababu mbali mbali.
2.1 Maana ya sanaa za maonyesho. (Jando, Unyago na Michezo ya watoto) 
Sanaa za maonyesho ni sanaa kongwe na muhimu katika fasihi simulizi. Kipera hichi kimeelezwa na wataalamu mbali mbali na kubainisha mambo muhimu yanayozibainisha katika utendaji wake. Wataalamu hao ni kama Semzaba, E (1997:1) Sanaa za maonyesho ni uonyeshi wa maisha kisanii ambapo mwonyeshaji na hadhira huwepo mahali pamoja na wakati mmoja. Katika fasili hii inabainika kuwa sanaa za maonyesho ni namna ya kuonyesha maisha kisanii ambapo mwonyeshaji na anaeonyeshwa huwa mahali pamoja kwa wakati mmoja katika tendo la uonyeshi huo. Kipera hiki pia kimeelezwa na kuwekwa bayana na Mulokozi, M (1996:187) Sanaa za maonyesho ni tukio au tendo la kijamii lenye sifa zifuatazo:- Dhana inayotendeka, uwanja wa kutendea, watendaji, hadhira, kusudio la kisanaa, muktadha wa kisanaa na ubunifu. Katika fasili hii Mulokozi anabainisha sifa za sanaa za maonyesho kwamba Sanaa za maonyesho haziwezi kuwa na kuitwa sanaa za maonyesho hadi ziwe na sifa mahsusi ambazo zinazipambanua na vipera vengine vya fasihi simulizi. Wataalamu wengine hawakuwa nyuma katika kufafanua Sanaa za maonyesho wakiwa na maana inayolingana na wataalamu Semzaba na Mulokozi. Miongoni mwao ni kama Fulgence, L. Mbunda (1996) yeye anasema kuwa “Sanaa za maonyesho ni mchezo, matendo mbali mbali mathalan ya waganga na maigizo juu ya vita, harusi au wakati wa ngoma. Mhando na Balisidia (1976:2) Sanaa za maonyesho ni kitendo chochote chenye sifa nne ambazo ni mchezo, mchezaji, uwanja wa kuchezea na watazamaji. Dhana ya sanaa za maonyesho ni kongwe katika jamii za kiafrika ikiwemo Tanzania. Kwa mujibu wa http://www.chomboz.blogspot.com. “Sanaa za maonyesho za asili yaani za jamii ambayo utamaduni wake ulikuwa haujaingiliwa na wakoloni (wageni) kugawanywa katika makundi matano mbazo ni (i) sherehe (ii) ngoma (iii) masimulizi ya hadithi (iv) kusalia miungu (v) majigambo.” Ingawa zipo aina nyengine za sanaa za maonyesho kama ngonjera, tamthilia, michezo ya watoto, jando, unyago, utani na nyenginezo zinaingia katika kundi la Sanaa za maonyesho kwa umbon lake la utendaji wa matendo ya dhati na yale ya kisanaa. Nukuu hii inatubainishia vipengele mbali mbali vilivyomo katika kipera hichi kama vilivyotajwa hapo juu. Miongoni mwao ni jando, unyago na michezo ya watoto.
2.2 Maana ya Jando
Kamusi la Kiswahili Fasaha (2010:129) linasema kwamba Jando ni pahali wanapowekwa watoto wa kiume wanapotahiriwa= chari au ni tendo la kumtahiri mtoto wa kiume.
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2004:128). Inaeleza Jando “ kumdi la wototo wanaume wanapotahiriwa na kufundishwa mambo ya utu uzima.” Fasili hii inatubainishia kwamba jamii nyingi duniani wanapowataarisha watoto wao wa kiume kuingia ukubwani huwapa mafunzo yatakayoweza kuwaongoza katika kipindi chote chao cha utuuzima. Pia katika kitendo hicho watoto wakiume hutahiriwa ili kukaribishwa ukubwani.
Haji A. I na wenzake (1981:75) wanatubainishia dhana hii ya Jando kwa kusema “Katika sehemu hii, kutokana na mila za jamii, watu huwa wanatambulishwa rasmi mabadiliko hayo. Mfano ngoma za jadi jando na unyago zimo katika jamii za Kiafrika. Ambapo jando kwa kawaida ilikuwa kwa wale wavulana ambao wameshakuwa wakubwa kiasi ambacho wanataka waelezwe majukumu yao kuhusu namna ya kuishi katika jamii kwa marika hayo waliyofikia. Umri hutafautiana kati ya jamii na jamii. Kwenye shughuli yenyewe huweko matendo ambayo ni maigizo ya mafunzo hayo wanayotakiwa wayapate.” Nukuu hii inatueleza maana halisi na matendo yanayofanyika katika jando kwa watoto wa kiume.
2.3 Maana ya Unyago.
Kwa mujibu wa Kamusi la Kiswahili Fasaha (2010:432) linaeleza kwamba Unyago ni mafunzo wanayopewa wasichana ya mila za jamii yao au ni ngoma ya vielelezo inayochezwa katika mafunzo hayo.
Pia Kamusi la Kiswahili Sanifu (2004:436). Linaeleza Unyago “ mkusanyiko wa vijana mahali maalumu ili kufundishwa mila za kabila au ngoma ya kuwafundisha wari mila za kabila lao.” Fasili hii inatuarifu kwamba kwa upande wa watoto wa kike tendo la kuwapa mafunzo ili waingie katika utuuzima huitwa Unyago.
Kadhalika wataalamu Haji, A. I na wenzake (1981:75) kwa kusema “Unyago kwa kawaida huchezewa wasichana ambao wamekwisha vunja ungo. Nao pia inakuwa ni sherehe ya kujua kwamba msichana fulani ameshatoka katika kundi la watoto na sasa yumo katika kundi la watu wazima. Humo huwemo mafunzo ambayo ndiyo yanayotakiwa katika jamii ili yaendelezwe au ayafanye huyo anayefikia umri huo.” Kwa hivyo maelezo hayo yanatafautisha baina ya Jando na Unyago kwamba ni sherehe za kuwafunza watoto wa kike na kiume wanapoingia katika kundi la watu wazima.
2.4 Ufafanuzi zaidi kuhusu Jando na Unyago. 
Kwa mujibu wa Kayombo, F (2014) katika blogsport yake ya kijamii anaeleza kwamba “ Jando na Unyago ilikuwa ni shule ya malezi bora kwa vijana ambao walikuwa wanahama toka rika ya watoto kuwa watu wazima.
Mafunzo ya jando kwa wavulana yaliendana na kutahiriwa na hata kwa wasichana katika baadhi ya makabila. Makabila maarufu katika utamaduni huu ni Wazaramo,Wamakonde, Wakrya, Wayao na makabila mengi ya mkoa wa Singida. Vijana waliwapatiwa mafunzo juu ya maadili bora, kuwaheshimu wakubwa, kuwa shupavu, uwajibikaji, majukumu ya kuilinda familia, ukoo na kabila.
Mafunzo ya Maisha kwa Vijana Kupitia Jando na Unyago. Mafunzo katika jando na unyago yalikuwa na nia ya kumuandaa kijana kuingia katika majukumu ya utu uzima. Wasichana walifundishwa jinsi ya kutunza nyumba, jinsi ya kutunza watoto, lakini pia lazima tuseme walifundishwa jinsi ya kufanya mapenzi na kumridhisha mume.”  Bila ya shaka kwa vile Zanzibar ni visiwa basi watu wake wanamchanganyiko changamano wa watu wenye asili mbali mbali yakiwemo makabila yaliyotajwa hapo juu na Bw. Kayombo,  F (2014) katika mtandao wake wa kijamii.
2.5 Maana ya michezo ya watoto.
Michezo ya watoto. Kwa mujibu wa  Haji, A. I na wenzake (1981:75) “ Shughuli ya kutawazishwa mkuu wa mji (chifu) shughuli za uganga, kusalia miungu na michezo mingi ya watoto kama bui, ngodani n.k pia ni aina za sanaa za maonyesho.”  Katika nukuu hii inabainika kuwa michezo ya watoto ni miongoni mwa Sanaa za maonyesho.
Dhana ya michezo ya watoto imajadiliwa pia na mtaalamu Haji, M. O. (2010:51). Michezo ya watoto ni michezo ambayo watoto wanacheza katika mazingira yao wanamoishi. Watoto hufanya hivyo kutokana na kuiga mambo ambayo wanayaona katika jamii wanayoishi. Kwa mfano watoto wanaweza kucheza mchezo wa Kinyuli, Kachiri, Chura mwanamatumbatu, Matango manemane n.k. Michezo hii yote huchezwa hapa petu Tanzania bara na Visiwani. Watoto wanapocheza michezo yao katika jamii huwapatia faida nyingi sana kama vile:-
kuimarika viungo vyao vya mwili kwani katika kucheza watoto huweza kukimbia au kutenda mambo mbali mbali ambayo husaidia kuimarisha viungo vya mwili, wakati huo pia hujipatia burudani inayoambatana na fasihi simulizi pamoja na hayo watoto pia hupata nafasi ya kujiona na wao kuwa ni sehemu ya jamii na wanaweza kufanya kazi ya ujasiri katika mazingira yao.
Hata hivyo wazazi wanapowaona watoto wanacheza vizuri hupata fursa katika nafasi zao na kujiona kuwa watoto wao wako katika afya njema na kwa hivyo watoto hujenga urafiki au uhusiano mwema baina ya watoto wanaocheza na wazee wao.
3.0  Kukua au kuimarika kwa Sanaa za maonyesho ( Jando, Unyago na Michezo ya watoto)  
Makala haya yana lengo la kueleza  Jando, Unyago na Michezo ya watoto katika kukuwa katika jamii za kizanzibari.
Jando na Unyago uliimarika kutokana na kwamba wanajamii wa nyakati zilizopita waliamini kwamba ni kama chuo cha kutoa mafunzo mbali mbali kwa vijana wa kike na kiume.
Mzee  Suleiman Abdalla Suleiman[1] anasema:-
 Mimi ninavyofahamu wari hufundishwa namna ya kuishi vizuri na mume pamoja na kumhudumia, kumtunza mume na watoto au familia kwa jumla na kijana wa kiume  barobaro hufundishwa jinsi ya kuishi vizuri na mke.    
                                                                                     - Mzee Suleiman Abdalla (Zanzibar,  2015).
Kwa hivyo wanajamii wa nyakati hizo walithamini na kutukuza harakati hizo kwa kuwa ilikuwa ni darasa tosha kwa watoto wao na kujenga jamii yao kwa kufuata mila na desturi zao.

Michezo ya watoto pia ilikuwa ni chuo cha watoto katika kujenga mashirikiano miongoni mwa jamii. Haya yamethibitishwa na mtaalamu Haji, M. O. (2010:51). “ Hata hivyo wazazi wanapowaona watoto wanacheza vizuri hupata fursa katika nafasi zao na kujiona kuwa watoto wao wako katika afya njema na kwa hivyo watoto hujenga urafiki au uhusiano mwema baina ya watoto wanaocheza na wazee wao.”
Kadhalika muktadha huo Bi Rahma Abass[2] anatuhakikishia kwa kusema:-
“Tulikuwa tunacheza uwanjani tukiwa watoto wa kila nyumba katika kijiji chetu Mchangani (Shamba). Nyumba ya mlezi wangu ilikuwa na duka mbele ya duka hili palikuwa na uwanja mkubwa ukimurikwa na karabai siku za mbaamwezi sheti kweupeee.. iliyokuwa karabai ikininginia kwenye kipenu cha gunia cha duka hili. Wazee wetu walikuwa wamejipumzisha barazani mwa nyumba zao za udongo wakitutazama na kuendelea na mazungumzo yao. Sisi tukicheza michezo mbali mbali na kuimba, nakumbuka mchezo wa “Ngoda ngadani na Kitambaachangu cheupe. Aliimba:- 
“ kitambaa chngu cheupe
Kinamadoa meupe
taishi miaka yote na dada Patima ubenduke
bendu!
na tena ubenduke
bendu! …….”
Kwa kweli ilikuwa raha natamani nirudi utoto sasa yale yote hayapo yametoweka too…  kwa watoto wetu  wa kisasa TV zimewateka hawana muda wa kucheza pamoja.” 
                                                                               - Bi Rahma Abass Madeweya (Zanzibar, 2015)
Katika maneno hayo tunaona mandhari iliyokuwepo wakati huo na namana jamii ilivyokuwa pamoja kuwalinda na kuwalea watoto wao kwa uangalifu uliokuwa mkubwa kabisa.
Kadhalika Jando na Unyago pamoja na Michezo ya watoto iliaminika kuwa ni hospitali ya uchunguzi wa maradhi pamoja na kuimarisha afya za watoto wao. Wari walipokuwa ndani walikuwa wakichunguzwa afya zao za mwili. Mfano mwanamke alikuwa akichunguzwa maradhi katika sehemu zao za siri mfano maradhi ya “Vikanga[3]” maradhi hayo walikuwa wakiangaliwa na Nyakanga na pale yanapobainika maradhi hayo hukatwa kwa viwembe na baadae hutiwa dawa za kienyeji na kupona. Iliaminika maradhi ya “Vikanga” ikiwa hayakuondoshwa mapema kwa kijana wa kike anaweza kuwa tasa au akibahatika kuzaa mtoto anatangulia (kufa). Pia kwa upande wa vijana wa kiume hupimwa urijali wao na pindipo anapoonekana ana matatizo basi hutibiwa ili aweze kummudu vyema mkewe atakapo oa. Kadhalika ilikuwa kwa vijana wa kiume hufanyiwa tohara (kutahiriwa) kama Mzee Abdalla Suleiman Abdalla anasema:-
“ Ngariba huwatahiri watoto kuwakata magovi yao ya uume wao kwa kutumia visu vidogovidogo ambavyo huwa maalumu kwa kazi hiyo tu. Walikuwa wakivishwa vishuka shingoni. Wakati wakiwa ndani huko walikuwa wakipikiwa vyakula mbali mbali vya asili kama vile uji wa mtama wakati wa asubuhi mpaka wakakatika jasho chururuuu… inapofika jioni wanachinjiwa kuku na wanakula wao pamoja na Ngariba na Nyakanga. Muda wote huo hukaa ndani hadi kupona majaraha yao.”
-Mzee Abdalla Suleiman Abdalla(Zanzibar, 2015)
Bi Halima Zaidi Sizamani[4] anasema kwa upande wa wari:-
“Ah! Mbona makubwa wajukuu wangu! haya yalikuwa siri! Tena siri kubwa hatukupaswa kuyasema hadharani lakni …….. mimi nilivyoona  wari huwekwa ndani hukoo hukaakaa huko hadi kufunzika mafunzo ya jamii kama vile masuala heshima na urembo kwa wanawake kama kutunga shanga na kusaga liwa na namna ya kujishughulikia wakati wa hedhi hupewa vitambaa maalumu wakati huo waliita Mrekani (Mbinda)[5] na walikuwa wakifundishwa namna ya kuitengeneza na kuivaa ili kuzuia hedhi bila ya kuonekana na kujuulikana kwamba yumo katika siku zake ”
-Bi Halima Zaidi Sizamani (Zanzibar, 2015)
            Kwa upande mwengine jando, unyago na michezo ya watoto ilitumika na kutendwa kama ni kuendeleza mila na desturi za jamii.
Bi Halima Zaidi Sizamani  anasema wakati wa majadiliano ya ana kwa ana
Wajukuu zangu Unyago ulikuwa ni chuo kikubwa kwa watoto waliokwisha vunjaungo kwani walifundishwa jinsi ya kuziendeleza mila na desturi kama vile kuepukana na kufanya machafu baada ya kuwa watu wazima, kuwa na nidhamu kwa waliowazidi kama kupokea mzigo wa mkubwa wake anapomuona amebeba mzigo huo na hasa mume kumpokea anapoingia ndani mwake wakiwa mume na mke. 
                                                - Bi Halima Zaidi Si Zamani ( Zanzibar, 2015)
Kwa hivyo mila na desturi zilisisitizwa kuendelezwa kwa wanajamii wote, na jamii ilirithisha mila na desturi hizo kupitia jando na unyago kizazi hadi kizazi.
Mzee Suleiman  Abdalla aliendelea kusema:-
“Baada ya siku kadhaa kupita katika Jando na Unyago wakati waliotahiriwa washapona majaraha yao na wari kumaliza mafunzo yao hutolewa nje. Siku wanapotolewa nje ilifanywa sherehe kubwa ambayo wazazi wa watoto waliowekwa Jandoni na Unyagoni walikuja kuwaona watoto wao wakiwa wamepona na wamefunzika pamoja na watu wengine walihudhuria sherehe hizo pakiwa na ngoma za asili na nyimbo zikitumbuiza. Kwa kweli ilikuwa inavutia. Sasa haya nadra kuyaona na wala hamyajui au mnayajua? Subutuuu…”
                                                                 -Mzee Suleiman  Abdalla (Kwamtipura, Zanzibar 2015)
Katika maneno haya tunagundua kuwa ngoma zilishiriki kutumbuiza wanajamii katika sherehe za jando na unyago na ndio ilikuwa kitambulisho cha jamii inayohusika ingawa kila jamii inatumia ngoma zao wakati wa sherehe mbali mbali. Kwa upande wa Pemba siku ya sherehe wari walipambwa kwa kuvishwa kanga mbili na baadae hupelekwa kila nyumba na kupiga hodi kwa majirani na kuamkia waliokuwemo na baadae hupewa zawadi kama pesa, kanga, nguo au vitambaa na vyenginezo..
Biyaya anasema:-  Biyaya[6]
Mimi baada ya kupata ukubwa nilipelekwa kwa Nyakanga mkubwa kwa jina maarufu la Bibi wa mbuzini” niliekwa ndani na kufunzwa kwa muda wa siku saba. Na siku ya kutolewa ilifanywa shehere ndani. Sherehe hii niliimbiwa nyimbo na kupigwa ngoma ya msondo.
Mfano wa nyimbo hizo ni:-
“Kwa mume kuna ngondo hakuna kitu cha bure
Kwa mume kuna ngondo hakuna kitu cha bure
hakuna kitu cha bure
hakuna kitu cha bure…”
 Kama yule aliyekuwa hasikii basi akiimbiwa kama ifuatavyo:-
“ Mwari wenu si mwari wee…. Mwari kinjenje ure..
Mwari wenu si mwari wee…. Mwari kinjenje ure..”
--Biyaya (Zanzibar 2015)
Wimbo huu huimbiwa kwa yule aliyekuwa hasikii  (akitumwa hataki hana heshima) ili asikie basi wazazi wanatanabahishwa wawe imara katika malezi ili kuzitunza mila na desturi za Zanzibar. Na hii inathibitisha kwamba Zanzibar mara nyingi watoto wa kike au wakiume hupewa mafunzo mmoja mmoja bila ya kukusanywa kwa pamoja kama iliyo kwa makabila mengine ya Tanzania bara. Ushahidi wa hayo Bw. Kayombo F (2014) katika blogsport yake ya kijamii anatuonesha picha zifuatazo:-
jando-na-unyago_unyago-1jando-na-unyago_mafunzo-maasai
Vijana Wakiwa katika Mafunzo ya Ujasiri na Kujihami Katika Jando (kulia) na Wasichana wakiwa Wamejifunika Mablanketi wakiwa Unyagoni (kushoto)

Kwa upande wa michezo ya watoto ilishajihisha kuimarisha mila na desturi za kizanzibar kwa kuwaeleza watoto kutenda matendo mema kama kuswali na mashirikiano katika jamii.
Biyaya anabainisha hili kwa kusema:-
Miye  nikumbukavo twekuwa tukicheza michezo mingi mfano kama Ntaka Sali. Na twekuwa tukiimba kama hivi:-
“ Ntakaswali wee…salaa ya umande swalaaa…
Nsimamie wee… salaa ya umande salaa…
Niinamiee wee… salaa. ya umande salaa…
Niinukie wee.. salaa. ya umande salaa….”
--Biyaya (Zanzibar 2015)
Kutokana na maudhui ya nyimbo hiyo ilifunza watoto ingawa walikuwa wakicheza tu mila na desturi zao ziliwataka waswali swala zote. Na namna ya kuswali ni hivyo kusimama, kurukuu, kusujudu na vitendo vyengine vinavyofanyika katika kuswali.

4.1 Kufifia au kufa kwa Jando, Unyago na Michezo ya watoto Zanzibar.
Inaaminika kwamba Jando, Unyago na Michezo ya watoto imefifia au kufa kiutendaji kwa mujibu wa mambo mbali mbali. Mambo haya yaliendelea kufifia kutokana na kuja kwa wakoloni. Ukoloni ulipokuja umeleta mabadiliko mbali mbali katika jamii za kiafrika na Tanzania ikiwemo Zanzibar. Mabadiliko hayo yalikuwa katika Nyanja mbali mbali kama vile  elimu, dini, mazingira na sayansi na teknolojia au utandawazi.  Haya yanathibitishwa na Kayombo, F (2014) katika blogsport yake ya kijamii pale alipoandika:-
 “Malezi ya vijana katika karne hii ya utandawazi in changamoto nyingi. Vijana wanakosa elimu juu ya ukuaji na mabadiliko ya mwili waoili waweze kujitambua na kuchukua hatua stahili katika maisha. Pia wanakosa elimu na ustadi wa kukabiliana na maisha kama wazai,kama wake au waume. Vitu ambavyo vilikuwa vikifanyika katika unyago na jando lakini sasa hivi hili halifanyiki kutokana na mila hizi kuachwa kwasababu ya mabadiliko ya mitindo yetu ya maisha inayoletwa na utandawazi. Utandawazi unatafsiriwa kuwa ni mfumo wa uhisiano wa kimataifa katika nyanja mbalimbali kama vile biashara, uchumi au siasa uliowezeshwa na maendeleo ya teknolojia ya habari yanayofanya mataifa kuwasiliana kiurahisi.”
Tukiichunguza ibara hapo hio inathibitisha kwamba sanaa za Jando, Unyago na hata Michezo ya watoto kwa kiasi fulani  zimepata athari kubwa kwa kukumbwa na wimbi la utandawazi kama tulivyoona hapo juu. Kwa muktadha huo basi hata Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa sehemu ya dunia haiwezi kukwepa wimbi hilo. Hivyo hivi sasa ufanyikaji wa sanaa hizi Zanzibar umebadilika tafauti na nyakati zilizopita.
Bi Rahma Abass anasema:-
“ Mimi bahati mbaya sikuchezwa kama walivyokuwa wakichezwa watoto wa jirani yangu tulipokuwa tukiishi Sogea, kwa sababu baba yangu yaani nyinyi babu yetu alikuwa ni mtu wa dini (Shehe). Ila niliwahi kuona mambo kama hayo wakati nipo mdogo sehemu ambayo ikiitwa Makaburimsafa[7]. Ilikuwa pana msitu wakati huo. kaka yangu alinipakia kwenye baskeli na akanambia twende kulee.. wakati huo tulisikia ngoma ikirindima tunakoelekea. Kwa mbali tulionekana na bibi mmoja aliyetoka katika uwa wa makuti akilalama kwa mayote kama “ wakamateni hao wakamateni hao si wanataka kuja huku..” kusikia hivyo tukazitimua mbio na baskeli yetu.”
                                                                                               - Bi Rahma Abass (Zanzibar, 2015)
Bila ya shaka maneno hayo yanatuhakikishia kwamba sehemu zilizokuwa zikitendwa Jando na Unyago zilikuwa ni maalumu mbali na makaazi ya watu. Na kwa muktadha huo sehemu hizo kwa wakati tulionao sasa zimebadilika kama tunavyoona badala ya Makaburimsafa sasa panaitwa Kibandamaiti na karibuni tu kumebadilika na kuitwa “Uwanja wa demokrasi” sio rahisi tena kufanywa jando na unyago kama uliyokuwa ukitendwa mwanzo kwa kuwa sasa ni viwanja na majumba ya watu wakiishi ndani yake, sio msitu tena.
Kadhalika utendwaji wa Jando na Unyago umebadili muelekeo katika nyakati hizi hapa Zanzibar. Kwa miaka ya sasa sio rahisi kusikia kuwa watoto wa kike au wa kiume wamewekwa mahali maalumu kwa kikundi wakifanyiwa Jando na Unyago badala yake wazazi wengi wa Kizanzibari wanapobaini watoto wao wamebaleghe huwapaleka kwa masomo wao ili kufundishwa yanayowakabili katika kipindi hicho cha mabadiliko. Na kwa upande wa watoto wa kiume hufunzwa hayo mara baada ya kutaka kuoa au hujifunza wenyewe kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo FaceBook , Twitter na WhatApp.  Maneno haya yanatiliwa mkazo kwa maswali mazito na Bw. Kayombo, F (2014) katika blogspot yake akisema:-
“ Hapo awali vijana walikuwa wakifundwa katika unyago na jando na makungwi walikuwa wakufunzi juu ya mambo haya na walikuwa na jukumu la kufanya haya kwa niaba ya wazazi na jamii husika. Lakini sasa hivi kungwi wa watoto wetu ni nani? Mitandao ya kijamii kama FaceBook ,twitter na WhatApp? TV na Video wanazoangalia usiku na mchana pengine hata bila mipaka? Je teknolojia hizi zinatoa mafunzo yanayotakikana katika jamii zetu? Haya yote ni maswali ambayo yanahitaji majibu na hatua za haraka.”  
Michezo ya watoto nayo imekubwa na wimbi la maendeleo ya sayansi na teknolojia. Watoto badala ya kucheza pamoja uwanjani wakitazamwa na wazazi wao vipenuni mwa nyumba zao, sasa hukimbilia katika televisheni kwa kuangalia katuni mbali mbali katika sehemu za mashamba ni mijini. Wakati wa usiku pia watoto hao hukimbilia katika masomo ya ziada (Tuishen) au madrasa za usiku hasa katika maeneo ya mijini. Mambo hayo huwa yanawakosesha muda watoto kucheza michezo yao kama ilivyokuwa ikichezwa na watoto zamani.
Kadhalika dini ni moja kati ya sababu zinazosababisha jando na unyago kufa Zanzibar. Katika jamii za kizanzibar kuna migongano mbali mbali inayohusu mila na dini. Jando na unyago ni mila za watu Zanzibar watu hao wakiwa na dini mbali mbali ikiwemo uislamu. Kwa namna moja ama nyengine unyago unaaminika kwamba ni mila potofu isiyofaa kuendelezwa kwa misingi ya kiislamu. Haya yanathibitishwa na Irene Brunotti katika Swahili Forum 12 (2005) katika mada yake isemayo “Ngoma ni uhuni? Ngoma za kisasa mjini Zanzibar.”  Alibainisha kwa kuandika
“Unyago hushirikisha wanaume na wanawake kama tushuhudiavyo leo. Katika uislamu ni kosa kubwa kwa mwanamme kuchanganika na mwanamke. Katika unyago huibwa nyimbo za matusi hili halikubaliki hata kiakili na kimaadili seuze sheria… kwa ujumla huzalikana na kupatikana katika mila hii ya unyago mambo mengi ambayo yanaghafiriana na sharia … Jamani tuache mila, desturi na ada hizo potofu na badalaya yake tushikamane na kuzifuata mila na desturi sahihi za uislamu.”[8]
Katika maandishi hayo tunaweza kugundua kwamba uislamu ni moja kati ya sababu zinazochangia kufa kwa jando na unyago Zanzibar kwa kuwa wanajamii wengi wa kizanzibar ni wailamu bila ya shaka mila na desturi zizoendana na uislamu hulazimika kuzipiga kumbo au kuzikataa.

5.1  Hitimisho
kwa vile Sanaa hizi (jando, unyago na michezo ya watoto) ni miongoni mwa Sanaa za maonyesho katika fasihi simulizi zilikuwepo zamani na kutendwa kwa hamasa kubwa na wanajamii wa Zanzibar. Bila ya shaka zilitoa mchango mkubwa kwa jamii hususan kwa watoto na vijana  kama tulivyoona hapo juu. Na sasa zinaonekana kufifia au kutoweka utendaji wake ama kufa kabisa katika jamii. Hivyo iko haja ya kuziendeleza na kuzitunza kiutendaji na kimaandishi ili ziweze kufaidisha jamii kizazi hadi kizazi.
Kwa kuwa hakuna jambo lisilo kasoro ulimwenguni bila ya shaka sanaa za jando na unyago haziwezi kukosa hilo kama vile:-
Kutoa mafundisho kwa watoto ambao hawajafikia umri unaofaa. Kufungia wasichana au mtoto wa kike (mwari) ndani kwa muda mrefu mpaka wapate mchumba n.k.
Marekebisho yanahitajika kwa pale panapohitajika. Mfano katika jando na unyago Mafunzo juu ya mabadiliko ya kibayolojia wakati wa kubaleghe kwa vijana na hatua za kuchukua na wakati muafaka wa kuchukua hatua hizo. Mafunzo juu ya kuishi kama baba au mama kihalali ama mume na mke katika ndoa. Mafunzo juu ya kulinda, kuitunza na kuijali familia, Uzalendo kwa familia,ukoo,kabila na taifa kwa ujumla ni mambo ya kuzingatiwa na kuendelezwa katika Sanaa hizi za jando na unyago.















MAREJEO 
BAKIZA. (2010). Kamusi la Kiswahili Fasaha. Kenya. Oxford University Press.
Haji, A I na wenzake. (1981). Misingi ya Nadharia ya Fasihi: Taasisi ya Kiswahili na Lugha za                                             
                                                Kigeni/Wizara ya Elimu Zanzibar. Sweden by Berlings, Arlov.
Haji, M. O. (2010). Vipera vya Fasihi Simulizi Tanzania. Kidato cha 1-4: Kiponda Street Zanzibar.                                 
                               Medu Press.
John, J & Mduda, F. (2011). Kiswahili Kidato cha Tano na Sita. Dar-es Salaam: Oxford University 
                                             Press
Kayombo, F (2014). Jando na Unyago:Nini Mbadala Katika Karne Hii ya Utandawazi?. Iliyoonekana kutoka http://bongoposts.com/jando-na-unyago-nini-mbadala-katika-karne-hii-ya-utandawazi/ tarehe 20/4/2015.
M, Mulokozi. M .(1996). Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam Tanzania: Chuo Kikuu Huria cha  
Mbunda, F. L .(1996). Mbinu za Kufundishia Lugha ya Kiswahili. Dar es Salaam, Tanzania: Chuo                                Kikuu Huria Cha Tanzania.   
Ndumbaro, E (2013) Sanaa za Maonesho  Kabla ya Ukoloni Afrika Mashariki na Mbinu Zilizotumika Kufifisha au Kuua Sanaa za Maonyesho hapa Nchini. Iliyoonekana kutoka http://chomboz.blogspot.com/2013/11/sanaa-za-maonesho.html . Tarehe 20/3/2015.
                                       
Semzaba, E .(1997). Tamthilia ya Kiswahili. Dar es Salaam, Tanzania: Chuo Kikuu Huria cha
                                Tanzania.    
TUKI. (2004). Kamusi la Kiswahili Sanifu. Kenya. Oxford Univerisity Press.   

             






[1] Mzee Suleiman Abdalla Suleiman  katika mahojiano tuliyofanya nae tarehe ( 4-4-2015) Kwake Kwamtipura. Mzee huyu ni mzaliwa wa Bwejuu sasa akiwa na umri wa miaka 98. Katika mahojiano yetu alitwambia kwamba aliwahi kufanyiwa jando.
[2] Bi Rahma Abass Madeweya katika mahojiano tuliyofanya naye tarehe (10-4-2015). Kwake Jang’ombe. Bibi huyu ni mzaliwa wa Mchangani Shamba mwenye umri wa miaka 55 sasa. Katika mahojiano yetu alitwambia kwamba aliwahi kucheza michezo ya watoto utotoni kwake.
[3] Vikanga- Ni ugonjwa wa sehemu za siri kama vijunjua hivi.
[4] Bi Halima Zaidi Sizamani – katika mahojiano tuliyofanya nae tarehe (20-3-2015) kwake Michenzani Jumba namba tano. Bibi huyu ana umri wa miaka 95 sasa, ni mzaliwa wa Donge. 
[5] Ni vazi maalumu linalotayarishwa kwa ajili ya kuvaa wanawake katika siku za hedhi ili kukinga hedhi isimuenee katika nguo zake.
[6] Bi Yaya katika mahojiano yetu naye tarehe (5-42015) Alikuja Unguja kwa kuwatembelea jamaa zake. Anakaa Kangagani mwenye umri wake  miaka 50.
[7]  Sasa panaitwa Uwanja wa Demokrasia (Kibandamaiti)
[8] Irene Brunotti aliichukua katika Nasaha za dini www.uislamu.org/uislamu/nasaha/nasaha6.html