Monday, April 27, 2015

KUIMARIKA NA KUTOWEKA KWA JANDO UNYAGO NA MICHEZO YA WATOTO ZANZIBAR



Kukua au kuimarika na kufifia au kufa kwa Sanaa za maonyesho.
(Jando, Unyago na Michezo ya watoto)
1.      Utangulizi
Sanaa za maonyesho zimekusanya vipengele mbali mbali, vipengele hivyo ni kama:- Sherehe mbali mbali (harusi, siasa), ngoma mabali mbali,  masimulizi ya hadithi,  kusalia miungu,  majigambo,  ngonjera, tamthilia, michezo ya watoto, jando, unyago, utani na nyenginezo. Vipengele hivyo kila kimoja kinamaana inayojipambanua na kipengelele chengine katika utendaji wake. Kadhalika sanaa za maonyesho namna zilivyokuwa zikitekelezwa zamani ni tafauti na zinavyotendwa sasa. Hali hii ya utendaji hubadilika kulingana na nyakati, husababishwa na mambo mbali kama vile maendeleo ya sayansi na teknolojia, dini, mitazomo ya watendaji (fanani na hadhira) na hata hali ya mabadiliko ya mazingira katika jamii zinazohusika. Sanaa za maonyesho au tendaji hutendwa kwa namna mbali mbali kulingana na jamii inayohusika.  Tanzania ikiwemo Zanzibar sanaa hizi za maonyesho hutendwa au hutekelezwa kwa namna tafauti na jamii nyengine nje ya Tanzania.  Katika Makala haya tutajadili na kufafanua namna Sanaa za maonyesho (Jando, Unyago na Michezo ya watoto) zilivyoshamiri hapo mwanzo na namna zinavyofifia au kufa kwa sababu mbali mbali.
2.1 Maana ya sanaa za maonyesho. (Jando, Unyago na Michezo ya watoto) 
Sanaa za maonyesho ni sanaa kongwe na muhimu katika fasihi simulizi. Kipera hichi kimeelezwa na wataalamu mbali mbali na kubainisha mambo muhimu yanayozibainisha katika utendaji wake. Wataalamu hao ni kama Semzaba, E (1997:1) Sanaa za maonyesho ni uonyeshi wa maisha kisanii ambapo mwonyeshaji na hadhira huwepo mahali pamoja na wakati mmoja. Katika fasili hii inabainika kuwa sanaa za maonyesho ni namna ya kuonyesha maisha kisanii ambapo mwonyeshaji na anaeonyeshwa huwa mahali pamoja kwa wakati mmoja katika tendo la uonyeshi huo. Kipera hiki pia kimeelezwa na kuwekwa bayana na Mulokozi, M (1996:187) Sanaa za maonyesho ni tukio au tendo la kijamii lenye sifa zifuatazo:- Dhana inayotendeka, uwanja wa kutendea, watendaji, hadhira, kusudio la kisanaa, muktadha wa kisanaa na ubunifu. Katika fasili hii Mulokozi anabainisha sifa za sanaa za maonyesho kwamba Sanaa za maonyesho haziwezi kuwa na kuitwa sanaa za maonyesho hadi ziwe na sifa mahsusi ambazo zinazipambanua na vipera vengine vya fasihi simulizi. Wataalamu wengine hawakuwa nyuma katika kufafanua Sanaa za maonyesho wakiwa na maana inayolingana na wataalamu Semzaba na Mulokozi. Miongoni mwao ni kama Fulgence, L. Mbunda (1996) yeye anasema kuwa “Sanaa za maonyesho ni mchezo, matendo mbali mbali mathalan ya waganga na maigizo juu ya vita, harusi au wakati wa ngoma. Mhando na Balisidia (1976:2) Sanaa za maonyesho ni kitendo chochote chenye sifa nne ambazo ni mchezo, mchezaji, uwanja wa kuchezea na watazamaji. Dhana ya sanaa za maonyesho ni kongwe katika jamii za kiafrika ikiwemo Tanzania. Kwa mujibu wa http://www.chomboz.blogspot.com. “Sanaa za maonyesho za asili yaani za jamii ambayo utamaduni wake ulikuwa haujaingiliwa na wakoloni (wageni) kugawanywa katika makundi matano mbazo ni (i) sherehe (ii) ngoma (iii) masimulizi ya hadithi (iv) kusalia miungu (v) majigambo.” Ingawa zipo aina nyengine za sanaa za maonyesho kama ngonjera, tamthilia, michezo ya watoto, jando, unyago, utani na nyenginezo zinaingia katika kundi la Sanaa za maonyesho kwa umbon lake la utendaji wa matendo ya dhati na yale ya kisanaa. Nukuu hii inatubainishia vipengele mbali mbali vilivyomo katika kipera hichi kama vilivyotajwa hapo juu. Miongoni mwao ni jando, unyago na michezo ya watoto.
2.2 Maana ya Jando
Kamusi la Kiswahili Fasaha (2010:129) linasema kwamba Jando ni pahali wanapowekwa watoto wa kiume wanapotahiriwa= chari au ni tendo la kumtahiri mtoto wa kiume.
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2004:128). Inaeleza Jando “ kumdi la wototo wanaume wanapotahiriwa na kufundishwa mambo ya utu uzima.” Fasili hii inatubainishia kwamba jamii nyingi duniani wanapowataarisha watoto wao wa kiume kuingia ukubwani huwapa mafunzo yatakayoweza kuwaongoza katika kipindi chote chao cha utuuzima. Pia katika kitendo hicho watoto wakiume hutahiriwa ili kukaribishwa ukubwani.
Haji A. I na wenzake (1981:75) wanatubainishia dhana hii ya Jando kwa kusema “Katika sehemu hii, kutokana na mila za jamii, watu huwa wanatambulishwa rasmi mabadiliko hayo. Mfano ngoma za jadi jando na unyago zimo katika jamii za Kiafrika. Ambapo jando kwa kawaida ilikuwa kwa wale wavulana ambao wameshakuwa wakubwa kiasi ambacho wanataka waelezwe majukumu yao kuhusu namna ya kuishi katika jamii kwa marika hayo waliyofikia. Umri hutafautiana kati ya jamii na jamii. Kwenye shughuli yenyewe huweko matendo ambayo ni maigizo ya mafunzo hayo wanayotakiwa wayapate.” Nukuu hii inatueleza maana halisi na matendo yanayofanyika katika jando kwa watoto wa kiume.
2.3 Maana ya Unyago.
Kwa mujibu wa Kamusi la Kiswahili Fasaha (2010:432) linaeleza kwamba Unyago ni mafunzo wanayopewa wasichana ya mila za jamii yao au ni ngoma ya vielelezo inayochezwa katika mafunzo hayo.
Pia Kamusi la Kiswahili Sanifu (2004:436). Linaeleza Unyago “ mkusanyiko wa vijana mahali maalumu ili kufundishwa mila za kabila au ngoma ya kuwafundisha wari mila za kabila lao.” Fasili hii inatuarifu kwamba kwa upande wa watoto wa kike tendo la kuwapa mafunzo ili waingie katika utuuzima huitwa Unyago.
Kadhalika wataalamu Haji, A. I na wenzake (1981:75) kwa kusema “Unyago kwa kawaida huchezewa wasichana ambao wamekwisha vunja ungo. Nao pia inakuwa ni sherehe ya kujua kwamba msichana fulani ameshatoka katika kundi la watoto na sasa yumo katika kundi la watu wazima. Humo huwemo mafunzo ambayo ndiyo yanayotakiwa katika jamii ili yaendelezwe au ayafanye huyo anayefikia umri huo.” Kwa hivyo maelezo hayo yanatafautisha baina ya Jando na Unyago kwamba ni sherehe za kuwafunza watoto wa kike na kiume wanapoingia katika kundi la watu wazima.
2.4 Ufafanuzi zaidi kuhusu Jando na Unyago. 
Kwa mujibu wa Kayombo, F (2014) katika blogsport yake ya kijamii anaeleza kwamba “ Jando na Unyago ilikuwa ni shule ya malezi bora kwa vijana ambao walikuwa wanahama toka rika ya watoto kuwa watu wazima.
Mafunzo ya jando kwa wavulana yaliendana na kutahiriwa na hata kwa wasichana katika baadhi ya makabila. Makabila maarufu katika utamaduni huu ni Wazaramo,Wamakonde, Wakrya, Wayao na makabila mengi ya mkoa wa Singida. Vijana waliwapatiwa mafunzo juu ya maadili bora, kuwaheshimu wakubwa, kuwa shupavu, uwajibikaji, majukumu ya kuilinda familia, ukoo na kabila.
Mafunzo ya Maisha kwa Vijana Kupitia Jando na Unyago. Mafunzo katika jando na unyago yalikuwa na nia ya kumuandaa kijana kuingia katika majukumu ya utu uzima. Wasichana walifundishwa jinsi ya kutunza nyumba, jinsi ya kutunza watoto, lakini pia lazima tuseme walifundishwa jinsi ya kufanya mapenzi na kumridhisha mume.”  Bila ya shaka kwa vile Zanzibar ni visiwa basi watu wake wanamchanganyiko changamano wa watu wenye asili mbali mbali yakiwemo makabila yaliyotajwa hapo juu na Bw. Kayombo,  F (2014) katika mtandao wake wa kijamii.
2.5 Maana ya michezo ya watoto.
Michezo ya watoto. Kwa mujibu wa  Haji, A. I na wenzake (1981:75) “ Shughuli ya kutawazishwa mkuu wa mji (chifu) shughuli za uganga, kusalia miungu na michezo mingi ya watoto kama bui, ngodani n.k pia ni aina za sanaa za maonyesho.”  Katika nukuu hii inabainika kuwa michezo ya watoto ni miongoni mwa Sanaa za maonyesho.
Dhana ya michezo ya watoto imajadiliwa pia na mtaalamu Haji, M. O. (2010:51). Michezo ya watoto ni michezo ambayo watoto wanacheza katika mazingira yao wanamoishi. Watoto hufanya hivyo kutokana na kuiga mambo ambayo wanayaona katika jamii wanayoishi. Kwa mfano watoto wanaweza kucheza mchezo wa Kinyuli, Kachiri, Chura mwanamatumbatu, Matango manemane n.k. Michezo hii yote huchezwa hapa petu Tanzania bara na Visiwani. Watoto wanapocheza michezo yao katika jamii huwapatia faida nyingi sana kama vile:-
kuimarika viungo vyao vya mwili kwani katika kucheza watoto huweza kukimbia au kutenda mambo mbali mbali ambayo husaidia kuimarisha viungo vya mwili, wakati huo pia hujipatia burudani inayoambatana na fasihi simulizi pamoja na hayo watoto pia hupata nafasi ya kujiona na wao kuwa ni sehemu ya jamii na wanaweza kufanya kazi ya ujasiri katika mazingira yao.
Hata hivyo wazazi wanapowaona watoto wanacheza vizuri hupata fursa katika nafasi zao na kujiona kuwa watoto wao wako katika afya njema na kwa hivyo watoto hujenga urafiki au uhusiano mwema baina ya watoto wanaocheza na wazee wao.
3.0  Kukua au kuimarika kwa Sanaa za maonyesho ( Jando, Unyago na Michezo ya watoto)  
Makala haya yana lengo la kueleza  Jando, Unyago na Michezo ya watoto katika kukuwa katika jamii za kizanzibari.
Jando na Unyago uliimarika kutokana na kwamba wanajamii wa nyakati zilizopita waliamini kwamba ni kama chuo cha kutoa mafunzo mbali mbali kwa vijana wa kike na kiume.
Mzee  Suleiman Abdalla Suleiman[1] anasema:-
 Mimi ninavyofahamu wari hufundishwa namna ya kuishi vizuri na mume pamoja na kumhudumia, kumtunza mume na watoto au familia kwa jumla na kijana wa kiume  barobaro hufundishwa jinsi ya kuishi vizuri na mke.    
                                                                                     - Mzee Suleiman Abdalla (Zanzibar,  2015).
Kwa hivyo wanajamii wa nyakati hizo walithamini na kutukuza harakati hizo kwa kuwa ilikuwa ni darasa tosha kwa watoto wao na kujenga jamii yao kwa kufuata mila na desturi zao.

Michezo ya watoto pia ilikuwa ni chuo cha watoto katika kujenga mashirikiano miongoni mwa jamii. Haya yamethibitishwa na mtaalamu Haji, M. O. (2010:51). “ Hata hivyo wazazi wanapowaona watoto wanacheza vizuri hupata fursa katika nafasi zao na kujiona kuwa watoto wao wako katika afya njema na kwa hivyo watoto hujenga urafiki au uhusiano mwema baina ya watoto wanaocheza na wazee wao.”
Kadhalika muktadha huo Bi Rahma Abass[2] anatuhakikishia kwa kusema:-
“Tulikuwa tunacheza uwanjani tukiwa watoto wa kila nyumba katika kijiji chetu Mchangani (Shamba). Nyumba ya mlezi wangu ilikuwa na duka mbele ya duka hili palikuwa na uwanja mkubwa ukimurikwa na karabai siku za mbaamwezi sheti kweupeee.. iliyokuwa karabai ikininginia kwenye kipenu cha gunia cha duka hili. Wazee wetu walikuwa wamejipumzisha barazani mwa nyumba zao za udongo wakitutazama na kuendelea na mazungumzo yao. Sisi tukicheza michezo mbali mbali na kuimba, nakumbuka mchezo wa “Ngoda ngadani na Kitambaachangu cheupe. Aliimba:- 
“ kitambaa chngu cheupe
Kinamadoa meupe
taishi miaka yote na dada Patima ubenduke
bendu!
na tena ubenduke
bendu! …….”
Kwa kweli ilikuwa raha natamani nirudi utoto sasa yale yote hayapo yametoweka too…  kwa watoto wetu  wa kisasa TV zimewateka hawana muda wa kucheza pamoja.” 
                                                                               - Bi Rahma Abass Madeweya (Zanzibar, 2015)
Katika maneno hayo tunaona mandhari iliyokuwepo wakati huo na namana jamii ilivyokuwa pamoja kuwalinda na kuwalea watoto wao kwa uangalifu uliokuwa mkubwa kabisa.
Kadhalika Jando na Unyago pamoja na Michezo ya watoto iliaminika kuwa ni hospitali ya uchunguzi wa maradhi pamoja na kuimarisha afya za watoto wao. Wari walipokuwa ndani walikuwa wakichunguzwa afya zao za mwili. Mfano mwanamke alikuwa akichunguzwa maradhi katika sehemu zao za siri mfano maradhi ya “Vikanga[3]” maradhi hayo walikuwa wakiangaliwa na Nyakanga na pale yanapobainika maradhi hayo hukatwa kwa viwembe na baadae hutiwa dawa za kienyeji na kupona. Iliaminika maradhi ya “Vikanga” ikiwa hayakuondoshwa mapema kwa kijana wa kike anaweza kuwa tasa au akibahatika kuzaa mtoto anatangulia (kufa). Pia kwa upande wa vijana wa kiume hupimwa urijali wao na pindipo anapoonekana ana matatizo basi hutibiwa ili aweze kummudu vyema mkewe atakapo oa. Kadhalika ilikuwa kwa vijana wa kiume hufanyiwa tohara (kutahiriwa) kama Mzee Abdalla Suleiman Abdalla anasema:-
“ Ngariba huwatahiri watoto kuwakata magovi yao ya uume wao kwa kutumia visu vidogovidogo ambavyo huwa maalumu kwa kazi hiyo tu. Walikuwa wakivishwa vishuka shingoni. Wakati wakiwa ndani huko walikuwa wakipikiwa vyakula mbali mbali vya asili kama vile uji wa mtama wakati wa asubuhi mpaka wakakatika jasho chururuuu… inapofika jioni wanachinjiwa kuku na wanakula wao pamoja na Ngariba na Nyakanga. Muda wote huo hukaa ndani hadi kupona majaraha yao.”
-Mzee Abdalla Suleiman Abdalla(Zanzibar, 2015)
Bi Halima Zaidi Sizamani[4] anasema kwa upande wa wari:-
“Ah! Mbona makubwa wajukuu wangu! haya yalikuwa siri! Tena siri kubwa hatukupaswa kuyasema hadharani lakni …….. mimi nilivyoona  wari huwekwa ndani hukoo hukaakaa huko hadi kufunzika mafunzo ya jamii kama vile masuala heshima na urembo kwa wanawake kama kutunga shanga na kusaga liwa na namna ya kujishughulikia wakati wa hedhi hupewa vitambaa maalumu wakati huo waliita Mrekani (Mbinda)[5] na walikuwa wakifundishwa namna ya kuitengeneza na kuivaa ili kuzuia hedhi bila ya kuonekana na kujuulikana kwamba yumo katika siku zake ”
-Bi Halima Zaidi Sizamani (Zanzibar, 2015)
            Kwa upande mwengine jando, unyago na michezo ya watoto ilitumika na kutendwa kama ni kuendeleza mila na desturi za jamii.
Bi Halima Zaidi Sizamani  anasema wakati wa majadiliano ya ana kwa ana
Wajukuu zangu Unyago ulikuwa ni chuo kikubwa kwa watoto waliokwisha vunjaungo kwani walifundishwa jinsi ya kuziendeleza mila na desturi kama vile kuepukana na kufanya machafu baada ya kuwa watu wazima, kuwa na nidhamu kwa waliowazidi kama kupokea mzigo wa mkubwa wake anapomuona amebeba mzigo huo na hasa mume kumpokea anapoingia ndani mwake wakiwa mume na mke. 
                                                - Bi Halima Zaidi Si Zamani ( Zanzibar, 2015)
Kwa hivyo mila na desturi zilisisitizwa kuendelezwa kwa wanajamii wote, na jamii ilirithisha mila na desturi hizo kupitia jando na unyago kizazi hadi kizazi.
Mzee Suleiman  Abdalla aliendelea kusema:-
“Baada ya siku kadhaa kupita katika Jando na Unyago wakati waliotahiriwa washapona majaraha yao na wari kumaliza mafunzo yao hutolewa nje. Siku wanapotolewa nje ilifanywa sherehe kubwa ambayo wazazi wa watoto waliowekwa Jandoni na Unyagoni walikuja kuwaona watoto wao wakiwa wamepona na wamefunzika pamoja na watu wengine walihudhuria sherehe hizo pakiwa na ngoma za asili na nyimbo zikitumbuiza. Kwa kweli ilikuwa inavutia. Sasa haya nadra kuyaona na wala hamyajui au mnayajua? Subutuuu…”
                                                                 -Mzee Suleiman  Abdalla (Kwamtipura, Zanzibar 2015)
Katika maneno haya tunagundua kuwa ngoma zilishiriki kutumbuiza wanajamii katika sherehe za jando na unyago na ndio ilikuwa kitambulisho cha jamii inayohusika ingawa kila jamii inatumia ngoma zao wakati wa sherehe mbali mbali. Kwa upande wa Pemba siku ya sherehe wari walipambwa kwa kuvishwa kanga mbili na baadae hupelekwa kila nyumba na kupiga hodi kwa majirani na kuamkia waliokuwemo na baadae hupewa zawadi kama pesa, kanga, nguo au vitambaa na vyenginezo..
Biyaya anasema:-  Biyaya[6]
Mimi baada ya kupata ukubwa nilipelekwa kwa Nyakanga mkubwa kwa jina maarufu la Bibi wa mbuzini” niliekwa ndani na kufunzwa kwa muda wa siku saba. Na siku ya kutolewa ilifanywa shehere ndani. Sherehe hii niliimbiwa nyimbo na kupigwa ngoma ya msondo.
Mfano wa nyimbo hizo ni:-
“Kwa mume kuna ngondo hakuna kitu cha bure
Kwa mume kuna ngondo hakuna kitu cha bure
hakuna kitu cha bure
hakuna kitu cha bure…”
 Kama yule aliyekuwa hasikii basi akiimbiwa kama ifuatavyo:-
“ Mwari wenu si mwari wee…. Mwari kinjenje ure..
Mwari wenu si mwari wee…. Mwari kinjenje ure..”
--Biyaya (Zanzibar 2015)
Wimbo huu huimbiwa kwa yule aliyekuwa hasikii  (akitumwa hataki hana heshima) ili asikie basi wazazi wanatanabahishwa wawe imara katika malezi ili kuzitunza mila na desturi za Zanzibar. Na hii inathibitisha kwamba Zanzibar mara nyingi watoto wa kike au wakiume hupewa mafunzo mmoja mmoja bila ya kukusanywa kwa pamoja kama iliyo kwa makabila mengine ya Tanzania bara. Ushahidi wa hayo Bw. Kayombo F (2014) katika blogsport yake ya kijamii anatuonesha picha zifuatazo:-
jando-na-unyago_unyago-1jando-na-unyago_mafunzo-maasai
Vijana Wakiwa katika Mafunzo ya Ujasiri na Kujihami Katika Jando (kulia) na Wasichana wakiwa Wamejifunika Mablanketi wakiwa Unyagoni (kushoto)

Kwa upande wa michezo ya watoto ilishajihisha kuimarisha mila na desturi za kizanzibar kwa kuwaeleza watoto kutenda matendo mema kama kuswali na mashirikiano katika jamii.
Biyaya anabainisha hili kwa kusema:-
Miye  nikumbukavo twekuwa tukicheza michezo mingi mfano kama Ntaka Sali. Na twekuwa tukiimba kama hivi:-
“ Ntakaswali wee…salaa ya umande swalaaa…
Nsimamie wee… salaa ya umande salaa…
Niinamiee wee… salaa. ya umande salaa…
Niinukie wee.. salaa. ya umande salaa….”
--Biyaya (Zanzibar 2015)
Kutokana na maudhui ya nyimbo hiyo ilifunza watoto ingawa walikuwa wakicheza tu mila na desturi zao ziliwataka waswali swala zote. Na namna ya kuswali ni hivyo kusimama, kurukuu, kusujudu na vitendo vyengine vinavyofanyika katika kuswali.

4.1 Kufifia au kufa kwa Jando, Unyago na Michezo ya watoto Zanzibar.
Inaaminika kwamba Jando, Unyago na Michezo ya watoto imefifia au kufa kiutendaji kwa mujibu wa mambo mbali mbali. Mambo haya yaliendelea kufifia kutokana na kuja kwa wakoloni. Ukoloni ulipokuja umeleta mabadiliko mbali mbali katika jamii za kiafrika na Tanzania ikiwemo Zanzibar. Mabadiliko hayo yalikuwa katika Nyanja mbali mbali kama vile  elimu, dini, mazingira na sayansi na teknolojia au utandawazi.  Haya yanathibitishwa na Kayombo, F (2014) katika blogsport yake ya kijamii pale alipoandika:-
 “Malezi ya vijana katika karne hii ya utandawazi in changamoto nyingi. Vijana wanakosa elimu juu ya ukuaji na mabadiliko ya mwili waoili waweze kujitambua na kuchukua hatua stahili katika maisha. Pia wanakosa elimu na ustadi wa kukabiliana na maisha kama wazai,kama wake au waume. Vitu ambavyo vilikuwa vikifanyika katika unyago na jando lakini sasa hivi hili halifanyiki kutokana na mila hizi kuachwa kwasababu ya mabadiliko ya mitindo yetu ya maisha inayoletwa na utandawazi. Utandawazi unatafsiriwa kuwa ni mfumo wa uhisiano wa kimataifa katika nyanja mbalimbali kama vile biashara, uchumi au siasa uliowezeshwa na maendeleo ya teknolojia ya habari yanayofanya mataifa kuwasiliana kiurahisi.”
Tukiichunguza ibara hapo hio inathibitisha kwamba sanaa za Jando, Unyago na hata Michezo ya watoto kwa kiasi fulani  zimepata athari kubwa kwa kukumbwa na wimbi la utandawazi kama tulivyoona hapo juu. Kwa muktadha huo basi hata Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa sehemu ya dunia haiwezi kukwepa wimbi hilo. Hivyo hivi sasa ufanyikaji wa sanaa hizi Zanzibar umebadilika tafauti na nyakati zilizopita.
Bi Rahma Abass anasema:-
“ Mimi bahati mbaya sikuchezwa kama walivyokuwa wakichezwa watoto wa jirani yangu tulipokuwa tukiishi Sogea, kwa sababu baba yangu yaani nyinyi babu yetu alikuwa ni mtu wa dini (Shehe). Ila niliwahi kuona mambo kama hayo wakati nipo mdogo sehemu ambayo ikiitwa Makaburimsafa[7]. Ilikuwa pana msitu wakati huo. kaka yangu alinipakia kwenye baskeli na akanambia twende kulee.. wakati huo tulisikia ngoma ikirindima tunakoelekea. Kwa mbali tulionekana na bibi mmoja aliyetoka katika uwa wa makuti akilalama kwa mayote kama “ wakamateni hao wakamateni hao si wanataka kuja huku..” kusikia hivyo tukazitimua mbio na baskeli yetu.”
                                                                                               - Bi Rahma Abass (Zanzibar, 2015)
Bila ya shaka maneno hayo yanatuhakikishia kwamba sehemu zilizokuwa zikitendwa Jando na Unyago zilikuwa ni maalumu mbali na makaazi ya watu. Na kwa muktadha huo sehemu hizo kwa wakati tulionao sasa zimebadilika kama tunavyoona badala ya Makaburimsafa sasa panaitwa Kibandamaiti na karibuni tu kumebadilika na kuitwa “Uwanja wa demokrasi” sio rahisi tena kufanywa jando na unyago kama uliyokuwa ukitendwa mwanzo kwa kuwa sasa ni viwanja na majumba ya watu wakiishi ndani yake, sio msitu tena.
Kadhalika utendwaji wa Jando na Unyago umebadili muelekeo katika nyakati hizi hapa Zanzibar. Kwa miaka ya sasa sio rahisi kusikia kuwa watoto wa kike au wa kiume wamewekwa mahali maalumu kwa kikundi wakifanyiwa Jando na Unyago badala yake wazazi wengi wa Kizanzibari wanapobaini watoto wao wamebaleghe huwapaleka kwa masomo wao ili kufundishwa yanayowakabili katika kipindi hicho cha mabadiliko. Na kwa upande wa watoto wa kiume hufunzwa hayo mara baada ya kutaka kuoa au hujifunza wenyewe kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo FaceBook , Twitter na WhatApp.  Maneno haya yanatiliwa mkazo kwa maswali mazito na Bw. Kayombo, F (2014) katika blogspot yake akisema:-
“ Hapo awali vijana walikuwa wakifundwa katika unyago na jando na makungwi walikuwa wakufunzi juu ya mambo haya na walikuwa na jukumu la kufanya haya kwa niaba ya wazazi na jamii husika. Lakini sasa hivi kungwi wa watoto wetu ni nani? Mitandao ya kijamii kama FaceBook ,twitter na WhatApp? TV na Video wanazoangalia usiku na mchana pengine hata bila mipaka? Je teknolojia hizi zinatoa mafunzo yanayotakikana katika jamii zetu? Haya yote ni maswali ambayo yanahitaji majibu na hatua za haraka.”  
Michezo ya watoto nayo imekubwa na wimbi la maendeleo ya sayansi na teknolojia. Watoto badala ya kucheza pamoja uwanjani wakitazamwa na wazazi wao vipenuni mwa nyumba zao, sasa hukimbilia katika televisheni kwa kuangalia katuni mbali mbali katika sehemu za mashamba ni mijini. Wakati wa usiku pia watoto hao hukimbilia katika masomo ya ziada (Tuishen) au madrasa za usiku hasa katika maeneo ya mijini. Mambo hayo huwa yanawakosesha muda watoto kucheza michezo yao kama ilivyokuwa ikichezwa na watoto zamani.
Kadhalika dini ni moja kati ya sababu zinazosababisha jando na unyago kufa Zanzibar. Katika jamii za kizanzibar kuna migongano mbali mbali inayohusu mila na dini. Jando na unyago ni mila za watu Zanzibar watu hao wakiwa na dini mbali mbali ikiwemo uislamu. Kwa namna moja ama nyengine unyago unaaminika kwamba ni mila potofu isiyofaa kuendelezwa kwa misingi ya kiislamu. Haya yanathibitishwa na Irene Brunotti katika Swahili Forum 12 (2005) katika mada yake isemayo “Ngoma ni uhuni? Ngoma za kisasa mjini Zanzibar.”  Alibainisha kwa kuandika
“Unyago hushirikisha wanaume na wanawake kama tushuhudiavyo leo. Katika uislamu ni kosa kubwa kwa mwanamme kuchanganika na mwanamke. Katika unyago huibwa nyimbo za matusi hili halikubaliki hata kiakili na kimaadili seuze sheria… kwa ujumla huzalikana na kupatikana katika mila hii ya unyago mambo mengi ambayo yanaghafiriana na sharia … Jamani tuache mila, desturi na ada hizo potofu na badalaya yake tushikamane na kuzifuata mila na desturi sahihi za uislamu.”[8]
Katika maandishi hayo tunaweza kugundua kwamba uislamu ni moja kati ya sababu zinazochangia kufa kwa jando na unyago Zanzibar kwa kuwa wanajamii wengi wa kizanzibar ni wailamu bila ya shaka mila na desturi zizoendana na uislamu hulazimika kuzipiga kumbo au kuzikataa.

5.1  Hitimisho
kwa vile Sanaa hizi (jando, unyago na michezo ya watoto) ni miongoni mwa Sanaa za maonyesho katika fasihi simulizi zilikuwepo zamani na kutendwa kwa hamasa kubwa na wanajamii wa Zanzibar. Bila ya shaka zilitoa mchango mkubwa kwa jamii hususan kwa watoto na vijana  kama tulivyoona hapo juu. Na sasa zinaonekana kufifia au kutoweka utendaji wake ama kufa kabisa katika jamii. Hivyo iko haja ya kuziendeleza na kuzitunza kiutendaji na kimaandishi ili ziweze kufaidisha jamii kizazi hadi kizazi.
Kwa kuwa hakuna jambo lisilo kasoro ulimwenguni bila ya shaka sanaa za jando na unyago haziwezi kukosa hilo kama vile:-
Kutoa mafundisho kwa watoto ambao hawajafikia umri unaofaa. Kufungia wasichana au mtoto wa kike (mwari) ndani kwa muda mrefu mpaka wapate mchumba n.k.
Marekebisho yanahitajika kwa pale panapohitajika. Mfano katika jando na unyago Mafunzo juu ya mabadiliko ya kibayolojia wakati wa kubaleghe kwa vijana na hatua za kuchukua na wakati muafaka wa kuchukua hatua hizo. Mafunzo juu ya kuishi kama baba au mama kihalali ama mume na mke katika ndoa. Mafunzo juu ya kulinda, kuitunza na kuijali familia, Uzalendo kwa familia,ukoo,kabila na taifa kwa ujumla ni mambo ya kuzingatiwa na kuendelezwa katika Sanaa hizi za jando na unyago.















MAREJEO 
BAKIZA. (2010). Kamusi la Kiswahili Fasaha. Kenya. Oxford University Press.
Haji, A I na wenzake. (1981). Misingi ya Nadharia ya Fasihi: Taasisi ya Kiswahili na Lugha za                                             
                                                Kigeni/Wizara ya Elimu Zanzibar. Sweden by Berlings, Arlov.
Haji, M. O. (2010). Vipera vya Fasihi Simulizi Tanzania. Kidato cha 1-4: Kiponda Street Zanzibar.                                 
                               Medu Press.
John, J & Mduda, F. (2011). Kiswahili Kidato cha Tano na Sita. Dar-es Salaam: Oxford University 
                                             Press
Kayombo, F (2014). Jando na Unyago:Nini Mbadala Katika Karne Hii ya Utandawazi?. Iliyoonekana kutoka http://bongoposts.com/jando-na-unyago-nini-mbadala-katika-karne-hii-ya-utandawazi/ tarehe 20/4/2015.
M, Mulokozi. M .(1996). Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam Tanzania: Chuo Kikuu Huria cha  
Mbunda, F. L .(1996). Mbinu za Kufundishia Lugha ya Kiswahili. Dar es Salaam, Tanzania: Chuo                                Kikuu Huria Cha Tanzania.   
Ndumbaro, E (2013) Sanaa za Maonesho  Kabla ya Ukoloni Afrika Mashariki na Mbinu Zilizotumika Kufifisha au Kuua Sanaa za Maonyesho hapa Nchini. Iliyoonekana kutoka http://chomboz.blogspot.com/2013/11/sanaa-za-maonesho.html . Tarehe 20/3/2015.
                                       
Semzaba, E .(1997). Tamthilia ya Kiswahili. Dar es Salaam, Tanzania: Chuo Kikuu Huria cha
                                Tanzania.    
TUKI. (2004). Kamusi la Kiswahili Sanifu. Kenya. Oxford Univerisity Press.   

             






[1] Mzee Suleiman Abdalla Suleiman  katika mahojiano tuliyofanya nae tarehe ( 4-4-2015) Kwake Kwamtipura. Mzee huyu ni mzaliwa wa Bwejuu sasa akiwa na umri wa miaka 98. Katika mahojiano yetu alitwambia kwamba aliwahi kufanyiwa jando.
[2] Bi Rahma Abass Madeweya katika mahojiano tuliyofanya naye tarehe (10-4-2015). Kwake Jang’ombe. Bibi huyu ni mzaliwa wa Mchangani Shamba mwenye umri wa miaka 55 sasa. Katika mahojiano yetu alitwambia kwamba aliwahi kucheza michezo ya watoto utotoni kwake.
[3] Vikanga- Ni ugonjwa wa sehemu za siri kama vijunjua hivi.
[4] Bi Halima Zaidi Sizamani – katika mahojiano tuliyofanya nae tarehe (20-3-2015) kwake Michenzani Jumba namba tano. Bibi huyu ana umri wa miaka 95 sasa, ni mzaliwa wa Donge. 
[5] Ni vazi maalumu linalotayarishwa kwa ajili ya kuvaa wanawake katika siku za hedhi ili kukinga hedhi isimuenee katika nguo zake.
[6] Bi Yaya katika mahojiano yetu naye tarehe (5-42015) Alikuja Unguja kwa kuwatembelea jamaa zake. Anakaa Kangagani mwenye umri wake  miaka 50.
[7]  Sasa panaitwa Uwanja wa Demokrasia (Kibandamaiti)
[8] Irene Brunotti aliichukua katika Nasaha za dini www.uislamu.org/uislamu/nasaha/nasaha6.html

1 comment: